Benki ya Equity Tanzania imezindua rasmi Zanzibar Supreme, kituo cha huduma maalum za Equity bank kinacholenga kutoa huduma za kifedha zenye uzoefu wa hali ya juu, ushauri wa kibiashara na mahusiano ya karibu na wateja, kinachopatikana Kijangwani, Mjini Magharibi Zanzibar. Hii ikiwa ni hatua muhimu katika mkakati wa benki hiyo wa kuimarisha huduma za kifedha, kupanua ujumuishaji wa kifedha na kusaidia ukuaji jumuishi wa uchumi wa Zanzibar.
Uzinduzi wa Kituo cha Zanzibar Supreme unaifanya Equity Bank Tanzania kufikisha matawi mawili Zanzibar, jambo linaloonesha imani ya benki hiyo katika fursa za ukuaji wa uchumi wa Zanzibar pamoja na dhamira yake ya kuendelea kuhudumia wananchi, wafanyabiashara, taasisi na wawekezaji kwa karibu zaidi. Uzinduzi huu wa kituo cha Zanzibar Supreme uliongozwa na Mh. Dr. Hamad Omar Bakar, Naibu waziri wa Fedha na Mipango ambaye alikua ni Mgeni rasmi.
Kituo cha Zanzibar Supreme kimeanzishwa kwa lengo la kuhudumia wateja wa hadhi ya juu, wajasiriamali wakati na wa kubwa, kampuni, sekta ya hoteli, wawekezaji, pamoja na wadau wengine muhimu kupitia huduma za kibenki za kiwango cha juu, zenye kuzingatia mahitaji ya mteja na uhusiano wa karibu kati ya benki na mteja.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Bank Tanzania, Bi. Isabela Maganga, alisema kufunguliwa kwa kituo hiki ni sehemu ya mkakati mpana wa benki hiyo wa kuwekeza katika huduma za kibenki zinazogusa sekta muhimu za uchumi na kuongeza upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha.
“Uzinduzi wa kituo cha Zanzibar Supreme ni hatua muhimu katika safari yetu ya kuendelea kusogeza huduma za kifedha karibu na wateja wetu. Kupitia kituo hiki, tunalenga kutoa huduma za kibenki zinazokidhi mahitaji ya wateja binafsi, wafanyabiashara wa kati na wakubwa, kampuni, wawekezaji na sekta ya hoteli, ambayo ni moja ya nguzo muhimu za uchumi wa Zanzibar,” alisema Bi. Maganga.
Aliongeza kuwa Equity Bank Tanzania itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya vituo vya hudum kwa wateja, huduma za kidijitali, na suluhisho za kifedha zinazosaidia ukuaji wa biashara, uwekezaji, upatikanaji wa mitaji, na uwezeshaji wa kifedha wa muda mrefu.
“Tunaamini kuwa taasisi za fedha zina jukumu muhimu katika kusaidia maendeleo ya kiuchumi kwa kutoa huduma zinazowezesha watu na biashara kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi. Kituo hiki ni sehemu ya dhamira yetu ya kusaidia ukuaji wa Zanzibar kupitia huduma bora, za kuaminika na zinazolenga mahitaji halisi ya wateja,” aliongeza uzinduzi huu pia unaendana na jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, za kuendeleza ukuaji endelevu wa kijamii na kiuchumi, kuongeza ushiriki wa wananchi na sekta binafsi katika uchumi, na kuwezesha mabadiliko chanya katika sekta za fedha na biashara kwa mwaka 2026 na kuendelea.
Kituo cha Zanzibar Supreme kitatoa huduma mbalimbali za kibenki ikiwemo kufungua akaunti, huduma za mikopo, huduma za biashara, huduma za fedha za kimataifa, huduma za kidijitali, ushauri wa kifedha, na huduma mahsusi kwa wateja wanaohitaji uangalizi wa karibu na suluhisho za kifedha zilizoboreshwa.
Hafla ya uzinduzi wa kituo hiki umewakutanisha viongozi wa Serikali, viongozi wa taasisi mbalimbali, wamiliki na watendaji wa hoteli, wafanyabiashara wakati na wakubwa, wawekezaji, wateja wa kimkakati na wadau wengine muhimu kutoka Zanzibar.
Kwa kufunguliwa kwa Zanzibar Supreme, Equity Bank Tanzania sasa ina jumla ya matawi 19 nchini, hatua inayozidi kuimarisha uwepo wake na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha katika maeneo muhimu ya kibiashara na ukuaji wa uchumi. Mtandao wa matawi ya Benki unajumuisha Makao makuu / Golden Branch, Golden Supreme, Quality Centre, Kariakoo, Mwenge, Ubungo, Mbagala, Temeke na Nyerere jijini Dar es Salaam, pamoja na matawi yaliyopo Arusha, Mwanza, Dodoma, Moshi, Mbeya, Morogoro, Geita, Kahama na Zanzibar, ikiwemo kituo cha Zanzibar Supreme kilichozinduliwa rasmi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Dkt. Hamad Omar Bakari (katikati) kwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania, Isabela Maganga (watatu kushoto) na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ali Maulid Juma wakizindua Kituo Kipya cha Zanzibar Suprime cha Benki ya Equity Tanzania, kilichopo eneo la Kijangwani, Zanzibar, Juni 6, 2026. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Equity, Prosper Nambaya, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Dkt. Said Haji Mrisho, Mteja wa Benki ya Equity, Dkt. Issa Seif Pamoja na Meneja wa Kituo cha Zanzibar Suprime, Anas Ramadhan.




.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...