Wadau wa sekta ya ushirika mkoani Dodoma wamekutana katika Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Dodoma kujadili utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa katika mikutano iliyopita, huku wakitathmini mafanikio yaliyopatikana na kuweka mikakati mipya ya kuimarisha vyama vya ushirika katika mkoa huo.

Akizungumza Juni 5, 2026, katika jukwaa hilo, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chintika, amesema jukwaa hilo ni la tano tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa kuwakutanisha wadau wa ushirika kwa lengo la kujadili maendeleo, changamoto na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Amesema ushirika wenye mafanikio unategemea ushiriki wa wanachama wake na kuwataka washiriki kutumia nafasi hiyo kujadili kwa uwazi masuala yanayoikabili sekta hiyo ili kupata suluhisho la pamoja.

Chintika amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha vyama vya ushirika vinakuwa imara, vinazingatia sheria na kanuni zilizowekwa na vinatoa manufaa kwa wanachama wake pamoja na jamii kwa ujumla.

Katika mjadala uliofanyika, wadau mbalimbali wameeleza kuwa bado kuna changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika, wamesema utekelezaji wa maazimio ya jukwaa hilo utasaidia kuimarisha utendaji wa vyama hivyo na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU), Fredy Lyimo, amesema kujenga uaminifu miongoni mwa wanachama, viongozi na watendaji ni hatua muhimu katika kuhakikisha vyama vya ushirika vinaendelea kuwa imara na endelevu, ameongeza kuwa utekelezaji sahihi wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya ushirika ni msingi wa mafanikio ya taasisi hizo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Climb Up Limited, Emmanuel Ngallah, ameeleza umuhimu wa matumizi ya teknolojia, na mizani janja ya kidigitali, katika shughuli za ushirika,itaweza kusaidia kuongeza uwazi, kurahisisha utunzaji wa kumbukumbu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama.

Mkoa wa Dodoma una zaidi ya vyama vya ushirika 130 vinavyohudumia sekta mbalimbali za uzalishaji na biashara, wadau wa jukwaa hilo wameeleza matumaini yao kuwa kupitia majadiliano na utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa, vyama hivyo vitaendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa mkoa huo.

Kaulimbiu ya Maendeleo ya Ushirika kwa mwaka 2026 inasema, “Ushirika kwa Dunia Yenye Amani; Linda Ushirika, Chagua Uadilifu,” ikisisitiza umuhimu wa maadili na uwajibikaji katika kuimarisha harakati za ushirika nchini.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...