Na Pamela Mollel,Arusha 

Jitihada za kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za nishati safi ya kupikia zimepewa msukumo mpya baada ya wadau kutoka sekta ya umma, binafsi na mashirika ya maendeleo kukutana jijini Arusha kujadili mikakati ya kuharakisha upatikanaji wa nishati hiyo nchini. Mkutano huo umejadili fursa, changamoto na mbinu za kuongeza matumizi ya teknolojia za kupikia ambazo ni salama kwa afya na mazingira.

Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, alisema Tanzania imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia, ambapo kiwango cha matumizi kimeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025. Alisema ongezeko hilo linaonesha namna juhudi za Serikali na ushirikiano wa wadau mbalimbali zinavyoendelea kuleta matokeo chanya katika kuboresha maisha ya wananchi.

Makamba alibainisha kuwa Serikali imeweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034. Alisema mkakati huo umejikita katika kuongeza upatikanaji wa teknolojia nafuu za kupikia, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi na kuhamasisha wananchi kubadili matumizi ya nishati za jadi zinazochangia uharibifu wa mazingira.

Alieleza kuwa mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa yamechangiwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo usambazaji wa mitungi 452,445 ya gesi ya LPG, majiko banifu zaidi ya 200,000 pamoja na mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia UNCDF. Miradi hiyo imewezesha mamia ya maelfu ya wananchi katika mikoa mbalimbali kupata huduma za nishati safi na salama ya kupikia.

Katika mkutano huo, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau, alitangaza kuwa EU imetenga euro milioni 30, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 92, kwa ajili ya kusaidia upanuzi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini. Alisema uwekezaji huo unalenga kuimarisha masoko ya nishati endelevu, kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa maeneo ya mijini na vijijini.

Grau alisema ufadhili huo ni sehemu ya mkakati wa Global Gateway unaolenga kuharakisha maendeleo endelevu kupitia uwekezaji katika sekta muhimu za kiuchumi. Alisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yana mchango mkubwa katika kulinda mazingira, kupunguza ukataji wa miti na kuboresha afya za wanawake na watoto ambao mara nyingi huathiriwa na moshi unaotokana na matumizi ya nishati za jadi.

Kwa mujibu wa wadau walioshiriki mkutano huo, ushirikiano kati ya Serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini. Walisema hatua zinazochukuliwa kwa sasa zinaipa Tanzania nafasi nzuri ya kufikia malengo yake ya mwaka 2034 huku zikichangia ustawi wa wananchi, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya uchumi wa taifa kwa ujumla.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...