Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma imeendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi kupitia Ofisi Inayotembea, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kodi na kuwasaidia walipakodi kutimiza wajibu wao kwa ufanisi.
Akizungumza wakati wa utoaji wa huduma hizo, Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Pendolake Elinisafi, amesema Ofisi Inayotembea ni sehemu ya mkakati wa TRA wa kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao ili kuwapatia huduma mbalimbali za kikodi bila kulazimika kufika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Ameeleza kuwa huduma zinazotolewa kupitia Ofisi Inayotembea ni pamoja na usajili wa Namba za Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), utoaji wa elimu ya kodi, ushauri wa masuala mbalimbali ya kikodi pamoja na utatuzi wa changamoto zinazowakabili walipakodi.
Elinisafi amewahimiza wananchi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma kutumia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma na maelezo sahihi yatakayowawezesha kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.
Makamu Mwenyekiti wa Soko la Wazi la Machinga Complex, Shaban Simba, amesema Ofisi Inayotembea imekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha upatikanaji wa TIN na namba za malipo (Control Number), jambo ambalo limewawezesha wafanyabiashara kulipa tozo za uendeshaji wa soko kwa urahisi na kwa wakati.
Aidha, amesema huduma hiyo imechangia kubadilisha mtazamo wa baadhi ya wafanyabiashara ambao hapo awali walikuwa na uelewa mdogo kuhusu masuala ya kodi, huku ikiwasaidia kufahamu wajibu wao na namna utozaji wa kodi unavyofanyika kwa mujibu wa sheria.
Naye mfanyabiashara wa soko hilo, Tatu Bilimo, amesema kuwa uwepo wa Ofisi Inayotembea umewarahisishia kupata huduma muhimu za kikodi moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara, hivyo kuokoa muda na gharama walizokuwa wakitumia kufuata huduma hizo katika ofisi za TRA.
Wafanyabiashara hao wameiomba TRA kuendelea kutoa huduma hiyo, wakieleza kuwa itachochea ushiriki mkubwa zaidi wa wafanyabiashara katika mfumo rasmi wa kodi na kuongeza mchango wao katika kukuza mapato ya Serikali na maendeleo ya taifa kwa ujumla.




.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...