Na.Sophia kingimali.
WITO umetolewa kwa wanahabari Nchini kuendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu masuala yanayohusu maendeleo ya bara la Afrika na kuhakikisha simulizi za Waafrika zinasimuliwa na Waafrika wenyewe.
Wito huo umetolewa Juni 4,2026 Jijini Dar es salaam na Mwandishi wa habari za uchunguzi na mtayarishaji wa filamu ya maandishi (documentary), David Hundeyin amesema Waafrika wanapaswa kuelewa kwa undani sababu zinazochangia matukio ya kisiasa yanayotokea barani humo badala ya kuamini kuwa yanachochewa na sababu za ndani pekee.
Amesema kuwa baadhi ya vyombo vikubwa vya habari vya kimataifa vinaendeshwa kwa kuzingatia maslahi ya nchi vinakotoka na hivyo huwasilisha habari kwa mtazamo unaoendana na malengo ya kisiasa ya mataifa hayo.
“Waandishi wa habari wanapaswa kutambua kuwa kila chombo cha habari kina mtazamo fulani. Ni muhimu kwa Waafrika kujenga uwezo wa kusimulia hadithi zao wenyewe na kuchambua taarifa wanazopokea kutoka vyanzo mbalimbali,” amesema.
Kwa upande wake Mwanazuoni na mchambuzi wa maswala ya maendeleo kutoka Zimbabwe Joshua Maponga Amesema kuwa bara la Afrika linapaswa kuwa makini na migogoro ya kijiografia na kisiasa kati ya mataifa makubwa duniani, akidai kuwa ushindani huo unaweza kuathiri mwenendo wa siasa na maendeleo katika nchi mbalimbali za Afrika.
Aidha, Maponga ametaka uchunguzi zaidi ufanyike kuhusu vyanzo vya fedha vinavyotumika na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), akisisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo.
Amesema serikali zinapaswa kuhakikisha mashirika yote yanayofanya kazi katika nchi zao yanaeleza kwa uwazi vyanzo vya mapato yao na namna fedha hizo zinavyotumika ili kuondoa mashaka yoyote kuhusu shughuli zao.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hoja zake hazilengi kuhalalisha vitendo vyovyote vinavyoweza kukiuka haki za wananchi, bali kuchochea mjadala kuhusu ushawishi wa maslahi ya nje katika masuala ya kisiasa na kijamii ya Afrika.


.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...