Na MWANDISHI WETU, Dar es Salaam


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM - Bara) Ndg Stephen Wasira, amewataka Watanzania kuhifadhi na kuishi kulingana na urithi wa Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza katika mahojiano maalumu, na ujumbe kutoka Serikali ya Angola, leo Juni 27, 2026. Wasira amemuelezea Mwalimu Nyerere kuwa kiongozi wa kipekee ambaye aliwaunganisha wananchi, alitawala kwa uadilifu mkubwa, na kuondoka madarakani bila kujilimbikizia mali.

Wasira alisema mojawapo ya sifa kuu za Mwalimu Nyerere ni uwezo wake wa kuwahamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika masuala muhimu ya kitaifa badala ya kuwa watazamaji ukiwemo ulinzi wa taifa lao.

“Aliwashirikisha watu wote. Akieleza sababu ya vita, akawaambia ‘vita hii ni yetu sote.’ kila Mtu alipoona kiongozi wake anamweleza wazi hivi ndivyo ilivyotokea, hivi ndivyo tulivyoamua…basi mtu alishiriki moja kwa moja,”alisema Wasira akirejea Vita ya Kagera.

Kuhusu urithi halisi wa Nyerere, Wasira alitaja mambo mawili makuu ambayo yanapaswa kulindwa kwa umakini.

“Jambo moja tunalolikumbuka na tunalojaribu kulihifadhi kati ya aliyotuachia ni Uhuru. Pili ni Umoja. Kwa sababu Umoja hapa ni kitu tunachojivunia sana, nchi isiyo na ukabila, ambapo watu wa makabila na dini tofauti wanaishi pamoja kwa amani.” Amesema.

Alisema sehemu iliyogusa zaidi katika mazungumzo hayo yalikuwa maelezo ya Wasira kuhusu maisha ya Mwalimu Nyerere baada ya kung’atuka madarakani.

“Vizazi vijavyo vitamkumbuka Mwalimu Nyerere kama mtu aliyepigania uhuru wa nchi yake. Aliongoza nchi yake kwa miaka 24 kama Rais, na akaondoka madarakani akaenda kijijini. Akarudi kuwa mkulima mdogo. Hakuwa na pesa. Hakuwa na akaunti benki nje wala ndani ya nchi. Ni mtu wa kipekee sana,” alisema.

Aidha, alisema Mwalimu Nyerere aliamini kwamba uhuru wa Tanganyika hauwezi kuwa matunda zaidi pasipo nchi zingine za bara hilo kuwa huru.

"Mwalimu Nyerere aliamini kwamba uhuru wa Tanganyika bila uhuru wa Afrika kwamba usingekamilika mpaka nchi zote za Afrika ziwe huru.

“Alitoa mchango mkubwa wa ukombozi hasa kwa nchi za Kusini mwa Afrika, na mwisho aliamini katika umoja wa Afrika jambo ambalo hadi anaondoka duniani hakuweza kulikamilisha,” alieleza.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...