Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma
SERIKALI imesema Kamati za Watu Wenye Ulemavu zilizoanzishwa katika ngazi za Mkoa, Wilaya, Vijiji na Mitaa zinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010, huku utekelezaji wa majukumu hayo ukifikia asilimia 52.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt Festo Ndugange alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Stella Ikupa Alex, aliyetaka kufahamu kama kamati hizo zinafanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt Ndugange amesema sheria imezipa kamati hizo jukumu la kufuatilia upatikanaji wa huduma muhimu kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo afya, elimu, ajira, ulinzi wa jamii pamoja na miundombinu jumuishi.
Aidha, kamati hizo zina wajibu wa kushauri Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri kuhusu masuala yanayohusu watu wenye ulemavu, kufuatilia utekelezaji wa mipango na bajeti zinazowahusu, pamoja na kupokea na kujadili changamoto zinazowakabili na kupendekeza ufumbuzi wake.
Katika hatua nyingine, Dkt Ndugange amesema kupitia kamati hizo, jumla ya watu wenye ulemavu 328,733 wametambuliwa nchini kote. Kati yao, wanaume ni 162,464 huku wanawake wakiwa 166,269.
Ameeleza kuwa utambuzi à sasa àhuo umeiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi zinazotumika katika upangaji, utekelezaji na ufuatiliaji wa huduma mbalimbali za kijamii kwa watu wenye ulemavu.
Serikali imeahidi kuendelea kusimamia na kuhakikisha kamati hizo zinafanya kazi kwa ufanisi na kwa kuzingatia matakwa ya sheria ili kuimarisha ustawi na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya taifa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...