Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mkataba wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Barabara ya Kitusha–Kinampanda–Kisana–Kisiriri umeshasainiwa, hatua inayofungua njia ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kubadilisha shughuli za usafiri na uchumi katika maeneo ya Wilaya ya Iramba.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo, Jumapili Juni 14, 2026, wakati akizungumza, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa Tarafa ya Kinampanda katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Amesema Serikali imekamilisha hatua muhimu ya upatikanaji wa fedha za mradi huo na kwamba changamoto iliyobaki sasa ni kukamilisha taratibu za kumpata mkandarasi atakayetekeleza ujenzi huo.

“Leo tunavyoongea, mkataba wa upatikanaji wa fedha umeshasainiwa. Kwa hiyo fedha si tatizo tena. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Halmashauri ambao walishuhudia kusainiwa kwa mkataba huo,” amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema barabara hiyo itaanzia Kitusha, kupita Kinampanda, Galangala, Kisana na kuunganishwa na Kisiriri kabla ya kuelekea Sibiti, hatua itakayorahisisha mawasiliano na usafirishaji wa watu na bidhaa katika ukanda huo.

Waziri Mkuu amesema mradi huo utatekelezwa kwa kiwango cha kisasa na unatarajiwa kuwa miongoni mwa barabara bora zaidi mkoani Singida.

“Barabara hii huenda ikawa moja ya barabara bora kuliko zote hapa mkoani Singida. Itakuwa ni barabara ya kisasa kweli kweli,” amesema.

Akitoa ufafanuzi wa hatua za utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Singida, Mhandisi Claver Mwinuka amesema tayari mchakato wa kumpata mshauri elekezi unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Amesema baada ya kukamilika kwa michoro na nyaraka za zabuni, Serikali itaanza mchakato wa kumpata mkandarasi huku matarajio yakiwa ni mkandarasi huyo kupatikana ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

Mhandisi Mwinuka amesema barabara hiyo ina urefu wa kilometa 38.5 na itajengwa kwa upana wa mita 9.5, tofauti na barabara nyingi za TARURA ambazo hujengwa kwa upana wa mita 8.5.

Aidha, amesema barabara hiyo itakuwa na taa zaidi ya 400 pamoja na vituo vya mabasi vya kisasa vitakavyoboresha huduma za usafiri kwa wananchi.

Wakati huohuo, Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya katika Tarafa ya Kinampanda kwa kupeleka gari jipya la wagonjwa (ambulance) katika Kituo cha Afya Kinampanda ndani ya wiki moja hadi mbili.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya kwa wananchi kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Kinampanda kupitia mpango wa Serikali wa kujenga vituo vya afya katika kila tarafa.

“Leo kama sehemu ya shukrani, nawaletea ambulance mpya. Itakuwepo hapa kituoni ili iweze kuwasaidia wananchi wa Kinampanda,” amesema.

Aidha, Dkt. Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa miradi mingine ya barabara katika Wilaya ya Iramba ikiwemo Shelui–Nkongilangi–Tulya–Kidaru, Mtoa–Mtekente–Urugu–Mlandala–Sepuka pamoja na Iguguno–Nduguti–Gumanga–Sibiti ambayo ipo katika hatua mbalimbali za usanifu na maandalizi ya utekelezaji.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...