Na Jawadu Kinyobwa - Dsm
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Wanafunzi wa sheria kujenga taaluma
zao katika misingi ya nidhamu, ubunifu na uzalendo ili waweze kufanikiwa
katika soko la ajira la kimataifa linalozidi kuwa na ushindani.
Akizungumza
leo Juni 5, 2026 katika hafla ya Siku ya Kazi na Taaluma ya Shule ya
Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema mafanikio ya kitaaluma
hayawezi kupatikana bila kuzingatia maadili hayo matatu muhimu.
Akifafanua
kuhusu nidhamu, amesema ubora si jambo la muda mfupi bali ni tabia
inayojengwa kwa kujifunza kwa bidii, kutunza muda, kuwa na hamu ya
kujifunza mambo mapya na kuzingatia maadili ya taaluma.
Amefafanua
kuwa, nidhamu inayojengwa kupitia mahakama za mfano, kazi za kitaaluma
na shughuli za msaada wa kisheria ndiyo msingi wa kukabiliana na
changamoto za taaluma katika ngazi za kitaifa na kimataifa.
Aidha,
kuhusu ubunifu, Waziri huyo amesema maendeleo ya teknolojia yamebadili
kwa kiasi kikubwa namna taaluma ya sheria inavyotekelezwa duniani.
Ametaja matumizi ya Akili Mnemba, mifumo ya kidijitali ya usajili na
teknolojia za kisheria kuwa miongoni mwa mabadiliko yanayounda upya
mazingira ya kazi za sheria.
Katika hatua
nyingine, amesisitiza umuhimu wa uzalendo, akieleza kuwa wao ni walinzi
wa utawala wa sheria na utawala bora hivyo wanapopata fursa ya kufanya
kazi katika taasisi za kimataifa au kampuni kubwa nje ya nchi,
wanapaswa kutumia maarifa na uwezo wao kuisaidia Tanzania kutambulika
vyema nje ya nchi.
Sambamba na hayo, Amesema
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
imeendelea kuimarisha sekta ya sheria na haki kupitia mageuzi ya mfumo
wa haki, matumizi ya teknolojia, uwekezaji katika miundombinu ya utoaji
haki na kuhamasisha mifumo mbadala ya utatuzi wa migogoro.
Awali,
akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mhe. Ridhiwani amesema
sekta ya sheria ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi
na kijamii kupitia mchango wa wataalamu wa sheria katika kulinda
maslahi ya taifa, kuimarisha utawala wa sheria na kusaidia mageuzi ya
kidijitali.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...