Chuo cha Ustawi wa Jamii kimewahamasisha wananchi kutumia huduma za ushauri na msaada wa kisaikolojia zinazotolewa na taasisi hiyo, huku kikisisitiza umuhimu wa afya ya akili na malezi bora ya watoto katika kujenga jamii yenye maendeleo endelevu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma Juni 17,2026, Mratibu wa Kituo cha Elimu na Msaada wa Kisaikolojia cha Chuo cha Ustawi wa Jamii, Rufina Ume, amesema kituo hicho kinatoa elimu, ushauri na msaada wa kisaikolojia kwa wanafunzi, watumishi na wananchi kwa ujumla.
Amesema huduma zinazotolewa zinahusisha ushauri wa mahusiano na ndoa, utatuzi wa migogoro, changamoto mbalimbali za kisaikolojia, elimu ya uraibu pamoja na marekebisho ya tabia.
“Kituo hiki pia kinatoa huduma za kuwafuata wananchi majumbani na katika maeneo yao ya kazi kwa wale wenye changamoto zinazowazuia kufika kituoni. Tunawahudumia pia watumishi wa sekta binafsi na umma kulingana na mahitaji yao.”
Ume amesema kituo hicho kilianzishwa rasmi mwaka 2007 ndani ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii iliyo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, kwa lengo la kutoa elimu na msaada wa kisaikolojia kwa wanafunzi na watumishi kabla ya kupanua huduma hizo kwa jamii nzima.
Ameeleza kuwa kwa sasa taasisi hiyo imekuwa ikiwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo yenye majanga kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya afya ya akili na kusaidia kujenga jamii yenye utulivu wa akili na uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya kila siku kwa ufanisi.
Aidha, amesema ushiriki wao katika Wiki ya Utumishi wa Umma unalenga kutoa elimu kwa wananchi na kuwawezesha kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu ustawi wa jamii, afya ya akili na huduma zinazotolewa na chuo hicho.
Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara, Desderio Wambura Fortunatus, amesema chuo hicho kimejikita katika kuandaa wataalamu watakaosaidia kujenga kizazi chenye maadili, afya bora ya akili na misingi imara ya maendeleo kuanzia utotoni.
Amesema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 yanategemea uwekezaji kwa watu kuanzia katika hatua za awali za ukuaji wao, jambo linalohitaji wataalamu wenye uwezo wa kusaidia familia na jamii katika malezi sahihi ya watoto.



.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...