NA MWANDISHI WETU, DODOMA
Taasisi, mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina hisa chache zimefanikiwa kuwasilisha gawio kwa serikali lenye thamani ya shilingi trilioni 1.3.
Uwasilishaji huo umefanyika Juni 30, 2026, katika Ikulu ya Dar es Salaam, ambapo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alihudhuria hafla hiyo .
Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti Taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda amesema, gawio la shilingi trilioni 1.3, ni udhihirisho wa uimara wa serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
"Tumeshuhudia taasisi na mashirika ya umma yakitoa gawio la shilingi trilioni 1.3, hizi ni fedha nyingi sana hasa unapoziingiza katika mzunguko wa shughuli za kiuchumi na uboreshaji wa huduma za kijamii, lazima zilete tija katika maisha ya wananchi," amesema Chatanda.
Sambamba na hilo, Chatanda amesema, mafanikio hayo hayawezi kutenganishwa na uongozi thabiti wa Rais Dk. Samia ambaye daima amekuwa akitoa maelekezo mazuri ya namna bora taasisi hizo zinapaswa kufanya katika kuhakikisha zinazalisha faida na kujitegemea badala ya kuwa tegemezi kwa serikali.
"Rais Dk. Samia amekuwa akizisisitiza taasisi na mashirika ya umma kuzalisha faida na kuepuka utegemezi, kuna baadhi ya taasisi na mashirika yalikuwa hayana uwezo hata wa kutoa gawio, lakini sasa wanatoa gawio baada ya kufanyia kazi maelekezo ya Rais wetu, hivyo, nampongeza sana Rais wetu kwa uongozi wake bora," amesema.
Ikumbukwe kuwa, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 ya shilingi trilioni 62.3, serikali inatarajia kutumia mapato ya ndani kwa asilimia 74.2 katika utekelezaji wake, hivyo, gawio hili ni sehemu ya kufanikisha utekelezaji wa bajeti ambao ni muhimu katika kufanikisha mipango ya serikali ya maendeleo kwa watu wake.
Naye, Rais Dk. Samia katika hotuba yake, amezielekeza taasisi hizo kuwa wabunifu ili kuongeza tija ya uzalishaji.
"Hatuwezi kujenga uchumi shindani kwa taasisi zinazofanya kazi kwa mazoea. Tunahitaji taasisi zinazopimwa kwa matokeo badala ya takwimu pekee," amesema Rais Dk. Samia.
Kimsingi, gawio na michango ya shilingi trilioni 1.327 kwa mwaka huu ni ongezeko la asilimia 30 kutoka trilioni 1.028 mwaka jana.
Katika kutambua mchango wake, Rais Dk. Samia alitunukiwa Tuzo Maalum ya kuwa "Kinara wa Mageuzi katika Kuimarisha Mifumo ya Usimamizi wa Mashirika ya Umma kwa Maendeleo Jumuishi na Ustawi wa Taifa - Gawio Day 2026".



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...