Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Paschal Inyasi Chinyele, amesema Serikali inaendelea kutekeleza hatua mbalimbali za kuboresha huduma za kijamii katika Kata ya Zuzu, akibainisha kuwa eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yanayokua kwa kasi hivyo linahitaji uwekezaji zaidi katika miundombinu ya msingi, hususan huduma ya maji.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kutoa changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa mkuu wa mkoa wa Dodoma Julai 13, 2026, uliofanyika eneo la Chididimo lililopo Kata ya Zuzu Halimashauri ya Jiji la Dodoma, amesema kupitia Mfuko wa Jimbo la Dodoma Mjini, licha ya kugawana fedha na Jimbo la Mtumba katika mwaka wa fedha uliopita.

Amesema waliweza kutenga shilingi milioni 20 kwa ajili ya kuchimba kisima cha maji katika Shule za Msingi Chang’ombe na Milioni 20 zingine walichimba kisima katika shule ya msingi Chididimo, huku fedha za ujenzi wa kibanda cha kisima zikiwa zimepatikana kupitia nguvu ya wananchi na Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatarajia kukamilisha miundombinu iliyobaki.

Mbunge huyo amesema upatikanaji wa maji ni kipaumbele kwa kuwa hakuna maisha bila maji, akisisitiza kuwa mradi huo utawanufaisha wananchi kwa kiasi kikubwa, aidha amesema Serikali imetoa shilingi milioni sita kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika Hospitali ya Nzinje na shilingi milioni 46 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari, hatua itakayopunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu na kukabiliwa na vihatarishi vinavyoweza kuathiri masomo yao ikiwemo utoro na mimba.

Awali, Diwani wa kata hiyo aliwasilisha changamoto zinazoikabili Zuzu na kuomba kukamilishwa kwa kipande cha barabara ya lami chenye urefu wa kilomita tano kinachoelekea Ring Road, ujenzi wa vivuko pamoja na soko la kisasa litakalowarahisishia wananchi kupata huduma za biashara karibu na makazi yao badala ya kutumia gharama kubwa za usafiri kufuata huduma hizo maeneo ya mbali.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula, amepongeza utaratibu wa Mkuu wa Mkoa wa kutembelea wananchi na kusikiliza changamoto zao moja kwa moja, akisema hatua hiyo imeongeza kasi ya upatikanaji wa ufumbuzi wa kero mbalimbali na wananchi kuwa karibu na serikali Yao.

Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Jiji la Dodoma limetenga shilingi milioni 50 kwa kila eneo kwa ajili ya kujenga masoko katika maeneo yasiyo na huduma hiyo, huku Kata ya Zuzu ikiwa miongoni mwa maeneo yatakayonufaika, amesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utachochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa Dodoma Mjini.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...