-Watuhumiwa 188 washikiliwa wakuhusishwa na dawa hizo,sheria kuchukua mkondo wake


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni maeneo mbalimbali nchini na kufanikiwa kukamata tani 22.6 za dawa za kulevya, lita 30.5 na kilogramu 19.94 za dawa tiba zenye asili ya kulevya. 

Pia, imeteketeza ekari 228.5 za mashamba ya bangi pamoja na tani 3.3 za bangi na mirungi huku ikiyashikilia magari sita, bajaji mbili na pikipiki 33 zilikamatwa kuhusiana na uhalifu huo wakati watuhumiwa 188 wamekamatwa kwa hatua za kisheria.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Julai 2,2026 Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema operesheni hiyo imefanyika kati ya Mei na Juni mwaka huu.

Amesema operesheni zilizofanyika Dar es Salaam zilifanikisha ukamataji wa kilogramu 19.94 za bidhaa zilizotambulishwa kama virutubisho vya lishe aina ya AFA CELL (Moringa Extract) katika eneo la mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. 

“Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa maabara, ilibainika kuwa bidhaa hizo zilikuwa na kiambata cha dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Prazepam. Bidhaa hizo ziliingizwa nchini kutoka Malaysia na zilikuwa zinaandaliwa kusafirishwa kwenda Barbados katika visiwa vya Karibiani. 

Amefafanua katika tukio hilo watuhumiwa Agustino Metusela Ismaely (30), mkazi wa Kimara; Zamia Harid Upunda (23), mkazi wa Bungoni, Ilala; na Habiba Ally Mziga (54), mkazi wa Mbezi Makonde walikamatwa.

“Prazepam ni dawa tiba yenye asili ya kulevya iliyopo katika kundi la benzodiazepine inayotumika kutibu magonjwa mbalimbali ikiwemo wasiwasi, msongo wa mawazo na kukosa usingizi. Endapo dawa hizi zitatumika kiholela au bila maelekezo ya daktari zinaweza kusababisha uraibu, kuharibu mfumo wa fahamu, mfumo wa upumuaji, kupoteza fahamu na hata kifo.”

Katika operesheni nyingine iliyofanyika mtaa wa Manyanya, Kinondoni, amesema zilikamatwa kilogramu 34.87 za mirungi iliyokuwa ikisafirishwa kwa kutumia gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 490 ECM kutoka Tarakea, mkoa wa Kilimanjaro. 

Amesema Mirungi hiyo iliyotokea nchini Kenya ilikuwa imefichwa kwa kuchanganywa na matenga ya nyanya ili kuficha uhalisia wa mzigo huo. Baada ya kufikishwa Dar es Salaam, ilishushwa katika eneo la kituo cha mafuta kilichopo mtaa huo kabla ya kuanza kusambazwa kwa kutumia usafiri wa bajaji yenye namba za usajili MC 361 CZV.

“Katika tukio hilo, walikamatawa watuhumiwa Mohamed Omary Mohamed (24), utingo na mkazi wa Tandale; Suleman Omary Suguti (34), dereva wa gari hilo na mkazi wa Tarakea, Rombo; na Deo Paschal Maratua (32), dereva wa bajaji na mkazi wa Tandale kwa Mtogole. 

“Mtuhumiwa Husseni Jumaa

Salimu (52), mkazi wa Dar es Salaam, ambaye anadaiwa kuwepo Nairobi, Kenya, anatafutwa kuhusiana na tukio hilo.”

Aidha amesema katika operesheni iliyofanyika eneo la ukaguzi wa mizigo la Bandari ndogo ya boti zinazotoa huduma kati ya Dar es Salaam na Zanzibar, zilikamatwa gramu 972.05 za mirungi zilizokuwa zikisafirishwa na mtuhumiwa Kalsam Abdurahman Sebbi (43), raia wa Kenya mwenye makazi yake Mombasa. 

Wakati wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam  zilikamatwa gramu 162.48 za heroin zilizomuhusisha mtuhumiwa Omary Miraji Mbonaeni.

Pia mkoani Arusha, zilikamatwa kilogramu 106.04 za dawa za kulevya aina ya mirungi zilizokuwa zikisafirishwa kwa kutumia gari aina ya Toyota Premio lenye namba za usajili T 853 ECX. 

Kamishina Jenerali Lyimo amesema katika tukio hilo, alikamatwa mtuhumiwa Goodluck Erasto Nyakaselula (35), mkazi wa Mbezi Beach, Dar es Salaam, ambaye ni mtaalam wa picha za kitabibu (Radiographer) katika Hospitali ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam.

Aidha, wilayani Same mkoani Kilimanjaro, eneo la kituo cha mabasi yaendayo mikoani, zilikamatwa kilogramu 240 za mirungi zikiwa zimefichwa ndani ya mabegi ya nguo. Katika tukio hilo, walikamatwa watuhumiwa Irene Obedi Sule na Eliasi Obedi Sule.

Kufuatia operesheni zilizofanyika katika mikoa mingine nchini, zilikamatwa tani 19.5 za bangi, tani 2.6 za mirungi, gramu 11.63 za heroin na kilogramu 40 za skanka. 

Aidha, tani 3.3 za bangi na mirungi pamoja na ekari 228.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika wilaya za Chamwino mkoa wa Dodoma, kijiji cha Mwengei kilichopo wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi na katika vijiji vya Busekeseke na Miembeni vilivyopo wilaya ya Sengerema na Geita.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...