Na Mashaka Mhando, Mbeya

VIWANJA vya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Mbeya vilitikiswa na shangwe na nderemo kufuatia mkutano mkubwa uliowakutanisha maelfu ya madereva wa bodaboda na bajaji wa Jiji hilo ana kwa ana na Mkuu wao wa Wilaya, Mhe. Solomon Itunda kuzungumzia amani na utulivu.

Mkutano huo, ambao ulitawaliwa na hali ya kirafiki na maelewano, haukuwa tu wa kutoa maagizo, bali ulikuwa ni jukwaa la kimkakati la kuwakumbusha vijana hao nafasi yao nyeti katika uchumi na usalama wa Jiji la Mbeya.

Akizungumza huku akishangiliwa na umati huo, Mhe. Itunda aliwaeleza madereva hao ukweli usiofichika kuwa wao ni injini muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mustakabali wa nchi.

Alisema kutokana na asili ya kazi yao ya kukutana na mamia ya wananchi kila siku, wana nguvu kubwa ya kujenga au kubomoa taswira ya jiji katika sekta ya usafiri kwa kuwaeleza tofauti na uhalisia wa nchi inavyoendeshwa.

Hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya, ambaye amekuwa akisifika na wananchi wa Mbeya kama 'Mzee wa busara', aliwasihi madereva hao wa bodaboda na bajaji kuendesha vyombo vyao kwa umakini mkubwa na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kunusuru maisha yao na ya abiria wao.

"Ndugu zangu wa bodaboda na bajaji, sisi ni watu wa Mbeya, tunapokuwa kazini tulinde amani yetu. Nyie mkiwa mabalozi, lakini pia ni vizuri mkalinda amani ya nchi kwa kuhubiri amani kwa abiria wenu," alisema Itunda.

Katika kile kilichoonyesha kutambua mazingira wezeshi ya biashara, Mkuu huyo wa Wilaya alitumia jukwaa hilo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mhe. Itunda aliweka wazi kuwa msingi imara wa amani, utulivu, na uhuru wa kiuchumi uliojengwa na Rais Samia ndio unaowapa vijana wengi fursa ya kujitafutia kipato mitaani bila bughudha.

Akifafanua kuhusu fursa za kiuchumi, DC Itunda aliwafafanulia wananchi hao kuwa awali mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji haikuwa ikiwafikia walengwa, lakini Rais Samia ameweka utaratibu mpya unaohakikisha kila kijana aliyekuwa kwenye kikundi ananufaika.

Aliwataka vijana hao, kama miongoni mwa wanufaika, kulinda fedha za mikopo wanayopewa na kuirejesha kwa wakati, ili asilimia hiyo 10 iweze kuwanufaisha vijana wengi zaidi wa Jiji hilo baada ya maboresho hayo makubwa.

DC Itunda aliwataka bodaboda hao kuunga mkono juhudi hizo za Rais kwa vitendo, huku wakiweka maslahi ya Tanzania mbele, ili kuhakikisha makundi ya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu yanawezeshwa na kuifanya Tanzania yenye watu milioni 65 kupiga hatua kiuchumi.

Hata hivyo, kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mhe. Itunda hakusita kugusa mshipa wa usalama. Aliwapa onyo na kuwasihi vijana hao kutokubali kutumika kama daraja la uhalifu. Aliwaomba wawe walinzi wa kwanza wa Jiji kwa kutoa taarifa za siri kwa vyombo vya dola mara wanapobaini watu wasioeleweka.

"Jiepusheni na makundi yenye mwelekeo wa kuvunja sheria. Ushirikiano wenu na Serikali ndiyo nguzo pekee itakayotuhakikishia Mbeya inabaki kuwa salama kwa maendeleo endelevu," alisisitiza Mhe. Itunda.

Kauli hizo za DC ziliingia vizuri masikioni mwa madereva hao, ambao kwa upande wao hawakuwa na hiyana. Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, viongozi wa bodaboda waliipongeza Serikali kwa kuendelea kuwathamini na kutatua changamoto zao.

Kama ishara ya kukubaliana na mwongozo wa DC Itunda, madereva hao waliweka ahadi nzito mbele ya mamlaka kuwa kuanzia sasa watakuwa mabalozi wazuri wa usalama barabarani, watafichua wahalifu wote wanaochafua taswira ya kazi yao, na watalinda amani ya Mbeya kwa nguvu zao zote.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...