SAME.

MKUU wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amewaonya wananchi wanaojihusisha na uchimbaji haramu wa madini ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa hakuna mtu au mwekezaji mwenye kibali cha kufanya shughuli za uchimbaji huo.

Amesema Serikali ya wilaya imeanza kuwachukulia hatua za kisheria, kwa lengo la kulinda vyanzo vya maji, mazingira na maslahi ya wananchi.

Hatua hiyo imekuja jana baada ya Kasilda, akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Madini na Bonde la Mto Pangani, kutembelea baadhi ya maeneo yanayofanyika uchimbaji haramu wa madini na kujionea uharibifu mkubwa wa mazingira katika vyanzo vya maji vilivyopo Kata ya Mhezi.

Kasilda alisema ni kosa kisheria kuanza shughuli za uchimbaji wa madini bila kuwa na leseni au kibali kutoka Ofisi ya Madini, pamoja na kufanya shughuli yoyote ndani ya umbali wa mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji bila kibali kutoka Bonde la Mto Pangani.

Alibainisha kuwa serikali imeanza kuwachukulia hatua wahusika wote ili kunusuru uharibifu wa mazingira na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na shughuli hizo haramu.

"Ni kosa kisheria kuanza kuchimba madini bila kuwa na leseni au kibali husika kutoka Ofisi ya Madini na kufanya shughuli yoyote ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji bila kibali kutoka Ofisi za Bonde. Wote wanaohusika tumeanza kuwashughulikia mara moja kwa lengo la kunusuru uharibifu na athari kubwa zinazoweza kutokea kutokana na uchimbaji huo haramu," alisema Kasilda.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...