Na Pamela Mollel,Arusha
Maandalizi ya kuupokea Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Arusha yamekamilika kwa asilimia 100, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za Mbio za Mwenge, kutembelea miradi ya maendeleo na kuhudhuria mkesha mkubwa wa burudani utakaofanyika Viwanja vya FFU Mworombo jijini Arusha
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, anasema maandalizi yote yamekamilika na wilaya ipo tayari kuupokea Mwenge wa Uhuru, huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu
Anasema Mwenge wa Uhuru utatembelea na kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha maendeleo na kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa wananchi
Mkude anasema mbali na miradi ya maendeleo, Mwenge wa Uhuru utaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya UKIMWI, malaria, rushwa, matumizi ya dawa za kulevya na utunzaji wa mazingira kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo, "Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo."
Aliongeza kuwa baada ya shughuli za mchana kukamilika, kutafanyika mkesha wa Mwenge wa Uhuru katika Viwanja vya FFU Mworombo, ambapo wananchi watapata burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiongozwa na Ali Kiba na Juma Nature
Aidha, aliwataka wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani kutumia fursa hiyo kushuhudia Mbio za Mwenge wa Uhuru, kutembelea miradi ya maendeleo pamoja na kushiriki mkesha huo utakaokuwa na burudani na ujumbe wa uzalendo
Mkude alisema matarajio ya Wilaya ya Arusha ni kuona wananchi wakijitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa jamii.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...