Na Vero Ignatus, Michuzi TV-Arusha
Serikali imeeleza kuwa ina matarajio makubwa kwa Mawakili wa Serikali katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,
Matarajio hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia Julai 15 hadi 17, 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Katimba amewataka Mawakili wa Serikali kuyatumia mafunzo hayo kuboresha utendaji wao wa kazi, ikiwemo kutoa ushauri wa kisheria, kuandaa na kupitia mikataba, kusimamia majadiliano ya kimkakati pamoja na kushughulikia mashauri kwa weledi na ufanisi.
Amesema Serikali inahitaji Mawakili wa Serikali wenye uwezo wa kuona mbali, kufikiri kimkakati na kutumia sheria kama nyenzo ya maendeleo ili kuhakikisha kila uamuzi wa Serikali unalinda maslahi ya Taifa, unakuza uchumi na kuchochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Imani yangu kwenu ni kubwa kuwa ninyi mliohudhuria mafunzo haya mtakuwa sehemu ya kizazi cha Mawakili wa Serikali kitakachoiwezesha Taifa kufikia matarajio makubwa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," amesisitiza Mhe. Katimba.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno, alisema mafunzo hayo yamewapa washiriki fursa ya kujadili na kujifunza masuala mbalimbali ya kimkakati yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ubunifu na ufanisi zaidi katika kulinda na kutetea maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Maneno alieleza kuwa mafunzo hayo yalijikita katika usimamizi wa majadiliano na mikataba ya kimkakati, usuluhishi wa migogoro, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), usimamizi wa vihatarishi vya kisheria (Legal Risk Management), pamoja na matumizi ya Akili Unde (AI) katika taaluma ya sheria.
Aidha, aliwataka Mawakili wa Serikali kuendelea kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA) 2026.
Pia aliwasisitiza kusoma na kutafakari kwa kina kitabu cha Mama Samia Doctrine of Law ili kuelewa falsafa ya uongozi wa Rais na kuongeza kasi pamoja na ubora katika uchakataji wa masuala ya kisheria, hususan upekuzi na uandaaji wa mikataba kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maslahi ya Taifa.
Mafunzo hayo ya Bespoke 2026 yalifanyika chini ya kaulimbiu "Repositioning State Attorneys for Strategic Legal Leadership in Realizing Tanzania Development Vision 2050," yakihusisha Mawakili wa Serikali kutoka Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa (RS na LGAs) kwa lengo la kuimarisha uongozi wa kisheria katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...