Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amefungua rasmi Kituo cha Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto (ECD) cha Mwanakwerekwe kilichofadhiliwa na Stanbic Bank Tanzania, sambamba na uzinduzi wa Mpango wa Zanzibar wa Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto wa Kisekta (2026–2031).

Ufadhili wa kituo hicho umetokana na awamu ya kwanza ya TZS milioni 350 iliyotolewa na Stanbic Bank Tanzania, ikiwa ni sehemu ya ahadi ya benki hiyo ya TZS milioni 500 kwa mpango wa Serikali wa Adopt an ECD unaoendeshwa na Shirika la Save the Children.

Kituo hicho kitatoa huduma bora za malezi na elimu ya awali kwa watoto wa wafanyabiashara na familia zinazofanya kazi katika Soko la Mwanakwerekwe na maeneo jirani.

“Uwekezaji huu unaakisi dhamira ya Stanbic Bank Tanzania ya kuendeleza malezi na makuzi ya awali ya mtoto kama msingi wa kujenga rasilimali watu, kukuza uchumi shirikishi na kuimarisha ustawi wa muda mrefu wa Zanzibar. Aidha, unaonesha mafanikio yanayowezekana pale Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo wanapounganisha nguvu kuelekea dira moja,” amesema Derick Lugemala, Afisa Mkuu wa Fedha, Stanbic Bank.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho, Mhe. Hemed aliipongeza Stanbic Bank kwa kuunga mkono ajenda ya serikali ya kuwekeza katika maendeleo ya mtoto katika umri wa awali na kuzitaka benki nyingine pamoja na taasisi za kifedha kuiga mfano huo wa kuchangia maendeleo ya taifa.

"Tunaipongeza Benki ya Stanbic kwa uwekezaji huu wa kimkakati na mchango wake endelevu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, si Zanzibar pekee bali Tanzania nzima kwa ujumla. Nazihimiza benki nyingine na taasisi za kifedha kuiga mfano huu mzuri wa kushiriki katika ujenzi wa taifa," alisema kabla ya kukifungua rasmi kituo hicho kilichopewa jina la Kituo cha Malezi ya Watoto cha Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (katikati), akimwakilisha Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, akikata utepe kuzindua rasmi Kituo cha Malezi ya Watoto cha Dkt. Hussein Ali Mwinyi kilichopo Mwanakwerekwe, Zanzibar. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Anna Athanas Maalim, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais  Ikulu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Saada Mkuya Salum, na Afisa Mkuu wa Fedha wa Stanbic Bank Tanzania, Derick Lugemala. Kituo hicho kimefadhiliwa  na Benki ya Stanbic kinacholenga kupanua upatikanaji wa huduma bora za malezi, makuzi na elimu ya awali kwa watoto nchini Zanzibar.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...