MAHAKAMA ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga imemuhukumu Isa Musini Rashidi maarufu kama Hamidu kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na htia ya kosa la kusafirisha kilo 75.15 za dawa za kulevya aina ya mirungi.Hukumu hiyo imesomwa hivi karibuni na Hakimu Mkazi Azizi Khamis, baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ambao uliweza kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote ya msingi.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Khamis alisema mahakama imeridhaka na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka na vielelezo ambapo wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
"Mahakama hii inakutia hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha Kifungu cha 16(1) na (2)(c) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, Marejeo ya Mwaka 2023, na inakuhukumu kifungo cha miaka 30 jela" alisema Hakimu Khamis.
Awali mahakamani hapo ilielezwa kuwa Aprili 10, 2026, katika eneo la Kinyatu ‘A’, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) walimkamata Isa akiwa anaendesha pikipiki nyeusi aina ya Huoniao yenye namba za usajili MC 569 EYG, akiwa amebeba mifuko miwili iliyokuwa na jumla ya mafungu 122 ya majani yaliyodhaniwa kuwa mirungi.
Uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali ulithibitisha kuwa majani hayo yalikuwa mirungi yenye uzito wa kilo 75.15.
Katika kuthibitisha shtaka, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano na vielelezo kumi huku mshtakiwa akikana tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Baada ya kuchambua ushahidi uliowasilishwa na pande zote, Mahakama iliridhika kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa thabiti na uliweza kuthibitisha kuwa mshtakiwa alikamatwa akiwa anasafirisha mirungi hiyo.
Mahakama pia iliridhika kuwa vielelezo vilihifadhiwa na kushughulikiwa kwa kufuata taratibu, kuanzia wakati wa ukamataji, uchunguzi wa kitaalamu hadi kuharibiwa kwa mujibu wa amri ya Mahakama.
Aidha, Mahakama imeamuru pikipiki aina ya Huoniao yenye namba za usajili MC 569 EYG, iliyotumika kusafirisha dawa hizo, itaifishwe na kuuzwa kwa mnada wa hadhara.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...