Na Mwandishi wetu, Arusha

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeshiriki Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma mwaka 2026 linaloendelea jijini Arusha, limewakutanisha wadau wa ununuzi pamoja na viongozi wa Serikali kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha Sekta ya ununuzi na ugavi nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando, Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Sheria PPAA, Bi. Agnes Sayi amewahimiza wadau wa ununuzi wa umma kutembelea banda la Mamlaka ya Rufani kupata uelewa juu ya majukumu na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo hususan matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST.

PPAA imeshiriki maonesho yanayofanyika pembezoni mwa Kongamano hilo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu uamuzi juu ya rufaa zinazotokana na mchakato wa ununuzi wa umma, uamuzi juu ya rufaa zinazotokana na kufungiwa kushiriki katika michakato ya ununuzi wa umma pamoja na uamuzi juu ya malalamiko yanayotokana na kushindwa kwa Afisa Masuuli kutoa uamuzi ndani ya muda uliowekwa.

Awali, akifungua Kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, (Mb.), Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila amesema sekta ya ununuzi wa umma inahusisha sehemu kubwa ya matumizi ya fedha za serikali, hivyo kuna ulazima wa kuhakikisha fedha zote zinazotengwa zinasimamiwa kwa umakini mkubwa ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Dkt. Nguvila amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mfumo wa ununuzi wa umma ili kuongeza uwazi, kupunguza gharama za ununuzi, kuharakisha mchakato na kurahisisha ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma.

"Ununuzi wa umma na ugavi ni nyenzo ya kisera na kimkakati ya Serikali katika kuchochea uzalishaji, ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira, kuimarisha kampuni za ndani, kukuza ubunifu, na kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wengi zaidi," amesema Dkt. Nguvila.

Kongamano hilo la siku tatu limeanza tarehe 29 - 31 Julai, 2026 limewakutanisha wadau wa ununuzi zaidi ya 1,500. Aidha, limewakutanisha Wakuu wa Taasisi, Maafisa Masuuli, Maafisa Ununuzi, Idara Tumizi, Maafisa Sheria, Wazabuni na Taasisi binafsi. 





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...