Na Mwandishi Wetu, Busan, Korea Kusini
KIONGOZI wa jadi wa Kimasai, Isack Lekisongo Meijo, ametoa wito wa kuwepo kwa uwiano endelevu kati ya binadamu, mifugo na wanyamapori katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ili kulinda urithi huo wa dunia na kuhakikisha maendeleo endelevu ya jamii za wafugaji.

Meijo alitoa kauli hiyo wakati wa mjadala uliofanyika sambamba na Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia cha UNESCO kilichofanyika Busan, Jamhuri ya Korea, ambapo Tanzania iliwasilisha taarifa kuhusu matokeo ya Tume mbili za Rais zilizochunguza masuala ya ardhi na uhamaji wa hiari wa wananchi kutoka Ngorongoro.

Alisema kwa vizazi vingi jamii ya Wamasai imeishi sambamba na wanyamapori huku ikichangia kuhifadhi mfumo wa ikolojia wa Ngorongoro, akisisitiza kuwa hakuna Ngorongoro bila Wamasai na hakuna Ngorongoro bila wanyamapori.

Akifafanua changamoto iliyopo, Meijo alifananisha Ngorongoro na ndege inayobeba wafugaji, mifugo na wanyamapori, akisema mzigo umeongezeka kupita uwezo wa eneo hilo. Alieleza kuwa ili safari iwe salama na endelevu, ni lazima kupunguza shinikizo kwa njia iliyopangwa na yenye uwiano.

Alisema ongezeko la watu, makazi, mifugo na wanyamapori ndani ya eneo lisiloongezeka ukubwa wake limeifanya mfumo wa matumizi mchanganyiko ya ardhi kukabiliwa na changamoto kubwa za uendelevu. Kwa mujibu wake, baadhi ya wadau wanaunga mkono uhamaji wa hiari wa wafugaji kwenda maeneo yenye fursa zaidi za kijamii na kiuchumi, huku wengine wakipendekeza kuhamisha wanyamapori ili kupunguza shinikizo kwa mazingira.

Meijo alisisitiza kuwa lengo kuu ni kulinda thamani ya kipekee ya Ngorongoro kama Urithi wa Dunia huku ukiimarisha maisha ya sasa na ya baadaye ya jamii ya Wamasai. Pia aliahidi kuwa jamii hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania, UNESCO pamoja na wadau wengine kuhakikisha uhifadhi, utamaduni na maendeleo endelevu vinaenda sambamba.

Katika mjadala huo, mjumbe kutoka Zimbabwe alihoji ni ipi kati ya kuhamisha wafugaji au kuhamisha wanyamapori inayobeba hatari kubwa zaidi. Akijibu kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania, Profesa Hamisi Malebo, alisema kuwa uhamaji wa hiari wa wananchi ni rahisi zaidi kuliko kuhamisha wanyamapori, jambo ambalo lina changamoto kubwa za kitaalamu, kifedha na kimazingira.

Washiriki kutoka mataifa 36 waliipongeza Tanzania kwa kuandaa mjadala huo, wakikubaliana kuwa ongezeko la watu, mifugo, migongano kati ya binadamu na wanyamapori pamoja na mabadiliko ya tabianchi vimeongeza shinikizo katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kwamba hatua za pamoja zinahitajika kulinda urithi huo wa dunia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...