Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imezindua "bulldozer" lenye thamani ya Shilingi milioni 450 katika Ranchi ya NARCO Ruvu, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa Ranchi hiyo, na kuongeza upatikanaji wa malisho, maji pamoja na kukuza uzalishaji wa mifugo nchini.

Akizungumza Leo Julai 20, 2026 Mkoani  Pwani, wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NARCO, Balozi Dkt. Aziz Ponary Mlima, amesema ununuzi wa "bulldozer" hilo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya DIRA ya Taifa ya 2050, huku akibainisha kuwa litasaidia kukabiliana na changamoto za malisho na maji ambazo zinawakabili wafugaji nchini.

"Bulldozer hili litatumika kuchimba visima vya maji, kuondoa vichaka vinavyozuia ukuaji wa malisho na kutengeneza mipaka ya Ranchi ili kudhibiti uvamizi, na Ranchi hii ya NARCO Ruvu ndiyo ya kwanza kunufaika na matumizi ya mashine hii ambayo pia itasaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji ndani ya ranchi za taifa." Amesema Dkt. Mlima

Balozi Dkt. Mlima ameongeza kuwa NARCO itaendelea kuwawezesha wawekezaji waliopo ndani ya Ranchi kwa kuwapatia huduma mbalimbali ikiwemo ukodishaji wa mitambo, hatua itakayoongeza tija ya uzalishaji na kuchangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali. 

Pia, Dkt. Mlima amewahimiza wafugaji kuwekeza katika mbegu bora za mifugo, madume bora, teknolojia ya uhimilishaji na matumizi ya viini tete ili kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Mohamedi Zuberi Mbwana, amesema malengo makuu ya ununuzi wa "bulldozer" hilo ni kuongeza na kuboresha nyanda za malisho, kukuza uzalishaji wa nyama kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kusaidia wafugaji kukabiliana na changamoto za malisho wakati wa kiangazi.

Aidha Mkurugenzi Mbwana, ametoa Rai Kwa wafugaji na wawekezaji kutumia "Bulldozer" hilo la NARCO ili waweze kubadili mfumo wao wa ufugaji Kwa kupanda malisho na kuondoa  vichaka. Vilevile Serikali imeazimia kuongeza tani za uuzaji wa nyama nje ya nchi kutoka tani 14000 Kwa sasa mpaka tani 50000 ifikapo mwaka 2030, NARCO inajukumu la kuongeza uuzaji huo wa nyama nje ya nchi.

Naye, mmoja wa wawekezaji katika Ranchi ya NARCO Ruvu, Bw. Mbambile Kisanjo, ameipongeza Serikali kwa kuleta "bulldozer" hilo akisema litasaidia kuboresha upatikanaji wa malisho, kutatua changamoto za mipaka, kuondoa vichaka na kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo, mambo ambayo yataongeza tija kwa wawekezaji na wafugaji wanaotumia ranchi hiyo.

Uzinduzi wa "bulldozer" hilo unaonyesha dhamira ya Serikali kupitia NARCO katika kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya ufugaji ili kuongeza tija, uzalishaji na mchango wa sekta ya mifugo katika ukuaji wa uchumi wa taifa, sambamba na kufanikisha malengo ya DIRA ya Taifa ya 2050.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...