Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mdhamini mkuu wa Ligi ya NBC Vijana chini ya Miaka 20 (NBC U20 Youth League), imekabidhi rasmi kombe la ubingwa wa msimu wa 2025/2026 kwa Azam FC (U20) baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga SC (U20) katika mchezo wa fainali uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, jijini Dar es Salaam.
Kabla ya mchezo huo wa fainali, Mbeya City FC (U20) ilitwaa nafasi ya tatu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya JKT Tanzania (U20), kufuatia timu hizo kutoka sare katika muda wa kawaida.Hafla ya kukabidhi kombe hilo iliongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Wajasiriamali, Vijana na Wanawake wa Benki ya NBC, Gaudence Shawa, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa soka nchini akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Nassor Idrissa, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Milambo, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya, viongozi wengine wa TFF pamoja na Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa, Taifa Stars, Miguel Gamondi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Shawa aliwapongeza mabingwa Azam FC (U20), washindi wa pili Yanga SC (U20), washindi wa tatu Mbeya City FC, vilabu vyote vilivyoshiriki, mabenchi ya ufundi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kufanikisha msimu ulioonyesha kiwango cha juu cha ushindani na maendeleo makubwa ya kiufundi.
Alisema ubora wa michezo ulioshuhudiwa msimu huu unaonesha wazi kuwa uwekezaji katika maendeleo ya soka la vijana unaanza kuzaa matokeo yanayotarajiwa, huku ukitoa matumaini makubwa ya kuimarika zaidi kwa ligi za ndani na timu za taifa katika miaka ijayo.
"NBC tunaamini kwamba mafanikio ya soka la kulipwa huanzia kwenye uwekezaji madhubuti katika maendeleo ya vijana. Ndiyo sababu tuliamua kuwa sehemu ya safari hii ya kujenga kizazi kipya cha wachezaji wenye uwezo wa kuleta ushindani mkubwa katika Ligi Kuu ya NBC, NBC Championship na hatimaye kuiwezesha Tanzania kuwa na timu za taifa zenye ushindani wa kimataifa. Tunafurahishwa kuona kiwango cha ushindani na ubora wa soka katika ligi hii vinaendelea kuimarika kila msimu, jambo linalotupa imani kuwa uwekezaji huu unaendelea kuleta matokeo chanya," alisema Shawa.
Aliongeza kuwa, kupitia udhamini wake wa Ligi Kuu ya NBC, NBC Championship na NBC U20 Youth League, benki hiyo itaendelea kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadau wengine wa mchezo huo katika kuimarisha mfumo wa ukuzaji vipaji, kuongeza ushindani wa ligi, kuinua hadhi ya soka la Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa sekta ya michezo kupitia ajira na fursa mbalimbali zinazotokana na mchezo huo.
"Soka limekuwa sekta muhimu ya kiuchumi inayogusa maelfu ya Watanzania. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza si tu katika mashindano, bali pia katika kujenga mfumo endelevu wa kuzalisha vipaji na kuongeza thamani ya mchezo huu kwa manufaa ya wachezaji, makocha, vilabu, mashabiki na taifa kwa ujumla," aliongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa DRFA, Lameck Nyambaya, aliipongeza NBC kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya soka nchini kupitia uwekezaji wake katika ligi za vijana.
Alisema mashindano ya msimu huu yameonesha mabadiliko makubwa katika ubora wa kiufundi, nidhamu ya mchezo na ushindani miongoni mwa timu zilizoshiriki, hali inayodhihirisha kuwa juhudi zinazowekwa katika kukuza soka la vijana zinaendelea kuzaa matunda.
"Tunashuhudia ongezeko kubwa la ubora wa wachezaji na ushindani kutoka klabu mbalimbali. Hii ni ishara kuwa Tanzania ipo kwenye mwelekeo sahihi wa kujenga msingi imara wa maendeleo ya soka kuanzia ngazi ya vijana. Tunatoa pongezi kwa NBC kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika eneo hili muhimu ambalo ndilo chimbuko la mafanikio ya soka letu," alisema Nyambaya.
Ligi ya NBC Vijana chini ya Miaka 20 imeendelea kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa TFF wa kuandaa kizazi kipya cha wachezaji wenye uwezo wa kuhimili ushindani katika ngazi za juu, huku udhamini wa NBC ukiendelea kuwa kichocheo muhimu katika kuboresha mazingira ya maendeleo ya vipaji na kuinua hadhi ya soka la Tanzania.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Nassor Idrissa (katikati) na Mkuu wa Kitengo cha Wajasiriamali, Vijana na Wanawake wa Benki ya NBC, Gaudence Shawa (kulia – alievaa suti) wakikabidhi kombe la Ligi ya NBC ya Vijana chini ya miaka 20 (NBC U20 Youth League) kwa nahodha wa timu ya Azam FC (U20) Rajabu Somvi baada ya timu hiyo kuwa bingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2025/2026. Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika jana katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es Salaam kufuatia mechi ya fainali baina ya mabingwa hao na wenzao Yanga SC (U20).
Wachezaji wa timu ya Azam FC (U20), viongozi na wadau mbalimbali wakijipongeza baada ya timu hiyo kukabidhiwa rasmi kombe la ubingwa wa Ligi ya NBC ya Vijana chini ya miaka 20 (NBC U20 Youth League) msimu wa 2025/2026. Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika jana katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es Salaam kufuatia mechi ya fainali baina ya mabingwa hao na wenzao kutoka Yanga SC (U20) mechi hiyo iliisha kwa timu ya Azam FC (U20) kuibuka na ushindi wa 2-1.
Kabla ya mchezo huo wa fainali, Mbeya City FC (U20) ilitwaa nafasi ya tatu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya JKT Tanzania (U20), kufuatia timu hizo kutoka sare katika muda wa kawaida.
Muonekano wa Kombe la Ligi ya NBC Vijana chini ya Miaka 20 (NBC U20 Youth League), msimu wa 2025/2026 kwa Azam FC (U20)
Wachezaji wa Azam FC (U20) na Yanga SC (U20) wakichuana kwenye fainali hiyo.
NBC Tunakuona Mbaaaaaaali kijana mwenye kipaji.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...