Na Janeth Raphael - Michuzi Tv 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yatategemea uwepo wa mfumo madhubuti wa sheria unaolinda maslahi ya nchi, kuimarisha utoaji wa haki na kuweka mazingira rafiki ya ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na maarifa, ubunifu na uwekezaji.

Akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali uliofanyika jijini Arusha leo, Rais Samia amesema wataalamu wa sheria wana jukumu kubwa la kuhakikisha mfumo wa kisheria unaendana na kasi ya maendeleo na mahitaji mapya ya taifa katika kipindi cha miaka 25 ijayo.

Ameeleza kuwa Tanzania inapoelekea kutekeleza Dira ya 2050, maeneo kama uchumi wa kidijitali, ulinzi wa taarifa na data, usimamizi wa rasilimali za madini, ardhi na bandari, pamoja na biashara za kikanda na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, yanahitaji sheria bora, sera zinazotabirika na mikataba yenye tija ili kuongeza ushindani wa uchumi na kuvutia uwekezaji.

Rais Samia amesema mabadiliko yanayoendelea duniani katika nyanja za uchumi na siasa yanapaswa kuwa chachu kwa wataalamu wa sheria kuongeza umakini katika kulinda maslahi ya taifa, rasilimali zake na kuhakikisha mikataba yote inazingatia manufaa ya Watanzania.

Aidha, amewataka mawakili wa Serikali kuendelea kusimamia utungaji na utekelezaji wa sheria zinazolinda uhuru wa nchi, haki za wananchi na mali za umma, huku akizitaka taasisi za Serikali kuimarisha mifumo ya kutambua na kudhibiti vihatarishi vya kisheria katika mikataba, manunuzi ya umma, miradi ya maendeleo, ardhi, TEHAMA, mazingira na utoaji wa huduma.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kutafsiri sheria mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao, hatua aliyoeleza kuwa itasaidia kuimarisha utawala wa sheria, uwajibikaji na ushiriki mpana wa wananchi katika maendeleo ya taifa.

Amesisitiza kuwa mfumo imara wa sheria si msingi wa utoaji wa haki pekee, bali pia ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu, ustawi wa uchumi na ulinzi wa maslahi ya Tanzania kwa vizazi vya sasa na vijavyo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...