Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema kitabu cha 'Falsafa ya Sheria ya Mama Samia' kinaakisi mchango mkubwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha utawala wa sheria kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Amesema hayo leo wakati akizindua kitabu hicho katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akimwakilisha Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba. Abdulla pia amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na mshikamano. "Bila amani, maendeleo hayatafanyika. Nawaomba wale wenye mawazo tofauti waungane na Watanzania wengine kuwa wazalendo na kulinda amani ya nchi yetu," amesema.
Akizungumzia maudhui ya kitabu, Abdulla amesema waandishi wake wamekitazama sheria kama mfumo unaogusa uchumi wa jamii nzima na sio kwa upana mdogo. Amesisitiza kuwa kitabu kimegusa maeneo matatu muhimu. La kwanza ni mapato ya ndani ambayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa kipindi cha awamu ya sita, na kusaidia serikali kugharamia miradi ya barabara, reli, umeme na afya.
La pili ni mageuzi ya VAT na kodi nyingine ambapo mapato yameongezeka na kuonesha kodi zinaendana na uchumi wa kidigitali. La tatu ni uwekezaji ambapo maboresho ya Sheria ya Uwekezaji ya 2022 yamerahisisha huduma na kuondoa urasimu. "Serikali ya awamu ya sita inataka uwekezaji unaozalisha ajira, unaoongeza teknolojia na ushiriki wa Watanzania katika uchumi," amesema Abdulla.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesema kitabu hicho kinaonesha jinsi sheria ilivyo chombo cha kuimarisha uchumi wa taifa na si cha udhibiti tu. "Sheria si maandishi tu bali ni miundombinu ya taifa. Ikiandikwa vibaya inaweza kuchelewesha maendeleo, ikiwa na utata inaleta migogoro, na ikiwa dhaifu inaleta matumizi mabaya ya mamlaka," amesema.
Johari amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuongoza nchi kwa mwelekeo wa maridhiano ili mageuzi ya uchumi, usawa na maendeleo yaweze kufikiwa.


.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...