Na Janeth Raphael MichuziTv
Vigogo wanane wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wameendelea kushikiliwa rumande baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi na rushwa inayowakabili bado haujakamilika.
Shauri hilo lilipotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma jana, Julai 9, 2026, Wakili wa Serikali, Gothard Mwingira, aliiambia mahakama kuwa upelelezi umefikia hatua za mwisho, lakini bado haujakamilika. Alieleza kuwa upande wa mashtaka unasubiri kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kabla ya kuendelea na hatua zinazofuata za shauri hilo.
Kutokana na maelezo hayo, upande wa Jamhuri uliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo wakati taratibu za upelelezi zikikamilishwa.
Washtakiwa katika shauri hilo ni aliyekuwa Rais wa CWT, Leah Ulaya, Rais wa sasa wa CWT, Suleiman Ikomba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maganga Japhet, Katibu Mkuu wa sasa, Joseph Misalaba, pamoja na Nashon Kidudu, Baraka Mbonalibha, Wambura Kihengu na Angelina Wambura. Pia kampuni ya Pyrite and Industries Company Limited inatajwa kama mshtakiwa katika kesi hiyo.
Viongozi hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Mei 25, 2026, ambapo walisomewa jumla ya mashtaka 14 yanayohusisha uhujumu uchumi na rushwa.
Hata hivyo, hawakutakiwa kujibu mashtaka hayo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kusikiliza kesi zinazohusu uhujumu uchumi.
Shauri hilo litaendelea kutajwa mahakamani baada ya upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi na kupata kibali kinachohitajika kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...