Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imesema imebaini uwepo wa vinywaji hasa Energy drinks nchini viambata vya kemikali ya THC ambayo hupatikana kwenye dawa za kulevya aina ya bangi ambavyo vilikuwa vinauzwa katika duka la Village Supermarket lililopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Julai 2,2026 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu operesheni zilizofanywa na Mamlaka hiyo katika kipindi cha Mei na Juni 2026, Kamishina Jenerali wa Mamlaka hiyo Aretas Lyimo amesema kupitia uchunguzi uliofanywa kwa kushirikiana na mamlaka nyingine wamebaini uwepo wa vinywaji vya Energy ambavyo vimechanganywa na bangi.
“Kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ulifanyika ukaguzi na uchunguzi wa bidhaa katika duka la bidhaa lijulikanalo kama “village supermarket” la jijini Dar es Salaam .
“Katika uchunguzi huo tumebaini uwepo wa vinywaji hususan “energy drinks” zenye viambata vya kemikali ya THC ambayo hupatikana kwenye dawa za kulevya aina ya bangi,”amesema
Amefafanua jumla ya kopo 122 zenye ujazo wa mililita 250 kila moja, sawa na lita 30.5 zenye chapa ya “TRIP” zilikamatwa. Watuhumiwa Syed Abdul Bast (43) raia wa Pakistan na Dhirendra Kumar Gorodhan (45), mtanzania mwenye asili ya Asia walikamatwa katika tukio hilo.
“THC ni kemikali inayopatikana kwenye dawa za kulevya aina ya bangi ambayo, ina madhara mbalimbali kwa mtumiaji ikiwemo, kuamsha magonjwa ya akili, kubadili utendaji kazi wa mfumo wa fahamu, kuchochea vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi, unyang`anyi, ukatili na kuchochea matumizi ya dawa nyingine za kulevya.”
Kutokana na kubaini uwepo wa vinywaji hivyo Kamishina Jenerali Lyimo amesema Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na mamlaka nyingine watafanya operesheni ya kuchunguza bidhaa katika maduka yote ili kuhakikisha bidhaa zilozopo ziko salama na hazina viashiria vya dawa za kulevya.
Alipoulizwa vinywaji vya Energy vilivyokutwa vimechanganywa na bangi zimetengenezwa wapi,amejibu vimetengenezwa katika viwanda vya nje ya Tanzania na vimeingizwa nchini kinyemela na hata katika karatasi zake waliotengeneza hawakuandika uwepo wa kemikali hizo.



.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...