Wananchi wa Kata ya Chang'ombe na Totowe, Wilaya Songwe Mkoa wa Songwe, wametakiwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kupambana na uhalifu, hususan vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wakati.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mh. Jabiri Makame, Julai 22, 2026, wakati wa ziara kampeni inayoitwa kwa jina la Serikali Nyumbani Kwako, ambapo alisisitiza kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto havikubaliki, huku akieleza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuwalinda, kuwatunza na kuwalea watoto kwa upendo kwa kuwa ndiyo msingi wa taifa la kesho.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, aliwataka wananchi kupiga vita matukio ya ubakaji na ulawiti katika maeneo yote, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kulinda watoto wa kike na wa kiume pamoja na kuheshimu haki na usalama wa watu wote katika jamii.
Aidha Kamanda Senga aliwasisitiza wananchi kupambana dhidi ya makosa hayo maana yanahitaji ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa za uhalifu kwa kuyazuia matukio hayo kabisa katika jamii.
Pia Kamanda Senga aliwataka wananchi kuachana na matumizi mabaya ya fedha kwa mambo yasiyo na tija na badala yake kuelekeza rasilimali katika kuboresha maisha ya familia, malezi ya watoto na shughuli za maendeleo.
Mwisho, Kamanda Senga alimalizia kwa kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia na kupambana na uhalifu, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kukomesha ubakaji, ulawiti, ulevi wa kupindukia na vitendo vingine vya kihalifu ili kujenga jamii salama, yenye amani na inayowalinda watoto.



.jpeg)





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...