Kinshasa, 17 Agosti 2026: Airtel Africa imeandika historia
baada ya kuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano barani Afrika kuzindua
kibiashara intaneti ya satelaiti kwa
simu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ikifungua ukurasa
mpya katika upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo yasiyofikiwa na minara ya
kawaida ya simu.
Huduma hiyo,
inayotolewa kupitia ushirikiano kati ya Airtel Africa na Starlink, inawezesha wateja
wenye simu janja zinazooana kupata huduma za mawasiliano katika maeneo ambayo
hayafikiwi na miundombinu ya kawaida ya mawasiliano ya simu.
Starlink ina
zaidi ya satelaiti 650 zinazosaidia huduma za mawasiliano ya moja kwa moja kati
ya satelaiti na simu (satellite-to-mobile). Kwa sasa, huduma hiyo
inalenga matumizi ya programu zinazotumia kiwango kidogo cha data, ikiwemo
ujumbe wa WhatsApp, pamoja na SMS, bila kuhitaji wateja kuwa na vifaa maalumu
au kifaa cha ziada.
Uzinduzi huo
unafuatia makubaliano ya kimkakati yaliyotangazwa na Airtel Africa na Starlink
mwezi Desemba 2025, pamoja na majaribio ya huduma za data na ujumbe nchini
Kenya mwezi Machi 2026.
DRC imekuwa soko
la kwanza la Airtel Africa na nchi ya kwanza barani Afrika ambako huduma ya intaneti ya satelaiti kwa simu (Starlink Mobile) imefikia hatua ya kutolewa
kibiashara.
Akizungumza
kuhusu uzinduzi huo, Afisa Mtendaji
Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema hatua hiyo ni muhimu katika
kupanua upatikanaji wa mawasiliano barani Afrika.
“Uzinduzi wa
kwanza kabisa wa kibiashara wa Starlink Mobile barani Afrika ni hatua muhimu
kwa Airtel Africa kupitia ushirikiano wetu na SpaceX. Kwa kuunganisha mtandao
wa Airtel wa ardhini na teknolojia ya satelaiti ya Starlink, tunapanua
upatikanaji wa mawasiliano muhimu zaidi ya mipaka ya miundombinu ya kawaida ya
simu. DRC inaongoza katika hatua hii muhimu ya maendeleo, na uzoefu
unaopatikana hapa utasaidia katika kupanua huduma hii hatua kwa hatua katika
masoko yetu, kwa kuzingatia idhini za mamlaka za udhibiti za kila nchi.
“Ninapenda
kutambua kwa namna ya pekee na kutoa shukrani zangu kwa Serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo kwa msaada wake muhimu katika kufanikisha hatua hii,
hususan kupitia Mheshimiwa Waziri wa Posta, Mawasiliano na Teknolojia Mpya ya
Habari na Mawasiliano, Rais wa Mamlaka ya Udhibiti pamoja na timu zao.”
Taldar alisema
uzoefu unaopatikana DRC utasaidia Airtel Africa katika kupanua huduma hiyo
katika masoko mengine ya kampuni, kwa kuzingatia idhini na matakwa ya mamlaka
za udhibiti katika kila nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel DRC, Thierry
Diasnoma, alisema huduma hiyo ya satelaiti itaongeza fursa za
mawasiliano katika nchi yenye eneo kubwa kijiografia, ambako baadhi ya wananchi
wanaishi, kufanya kazi au kusafiri mbali na miundombinu ya kawaida ya
mawasiliano.
“Huduma hii ya intaneti ya satelaiti kwa simu inatoa safu ya ziada ya mawasiliano,
ikisaidia wateja kuendelea kupatikana, kupata taarifa na kuwasiliana katika
maeneo ambayo mtandao wa minara haupatikani,” alisema Diasnoma.
Huduma ya intaneti ya satelaiti kwa simu inalenga pia kuwasaidia wasafirishaji na
kampuni za usafirishaji na usambazaji, mashirika ya kibinadamu, wahudumu wa
afya, wakulima, kampuni za uchimbaji madini na jamii zinazoishi katika maeneo
ambayo hayajafikiwa kikamilifu na mitandao ya ardhini.
Aidha, teknolojia
ya intaneti ya satelaiti kwa simu
inaweza kuwa nyenzo muhimu katika mawasiliano ya dharura wakati wa majanga ya
asili au pale ambapo mtandao wa kawaida unakatika kwa muda.
Kwa sasa, wateja
wanaotaka kutumia huduma hiyo wanapaswa kuwa na simu janja ya Android yenye LTE
inayooana na mfumo wa Starlink Mobile, pamoja na kifurushi cha data cha Airtel
DRC kinachokidhi vigezo au huduma ya data roaming iliyowashwa.
Airtel imesema
simu na vifaa vya kampuni ya Apple, vitawezeshwa kutumia huduma ya intaneti ya satelaiti kwa simu katika
siku zijazo.
Wateja wanaokidhi
vigezo wanaweza kujisajili kupitia MyAirtel
App na kupata huduma ya majaribio bila malipo kwa siku 30 za kwanza.
Wateja wanaosafiri
kwenda DRC na kujiunga na Airtel DRC wanaweza pia kujisajili kwa huduma hiyo ya
majaribio baada ya kuamilisha huduma inayokidhi vigezo na kupakua MyAirtel App.
Baada ya kipindi
cha majaribio, huduma itaendelea kupatikana kupitia vifurushi vya data vya
Airtel vinavyokidhi masharti.
Airtel Africa na
Starlink zimesema zinaendelea kuboresha huduma hiyo, huku uwezo wa ziada
ukitarajiwa kuongezwa kadri teknolojia inavyoendelea kukua na idhini za
udhibiti zinavyopatikana.
Uzinduzi huo
unaiweka Airtel Africa katika nafasi ya kampuni ya kwanza ya mawasiliano barani
Afrika kuanza kutoa intaneti ya
satelaiti kwa simu kibiashara, huku ikiendelea kutumia teknolojia mpya
kupanua wigo wa mawasiliano na kuongeza ujumuishwaji wa kidijitali barani
Afrika.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...