Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Benki ya Ushirika Tanzania (COOP BANK) imeweka mkakati wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo kwa kuwawezesha wakulima kupata teknolojia za kisasa, zana bora za kilimo pamoja na pembejeo zitakazosaidia kuongeza uzalishaji na kukuza kilimo biashara nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Ushirika, Godfrey Ng’urah, amesema benki hiyo imelenga kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo ili kuleta mabadiliko chanya katika uzalishaji, hasa kwa kuwawezesha wakulima na vyama vya ushirika kupata vifaa muhimu vya kisasa kwa gharama nafuu.

Amesema hatua hiyo imeanza kutekelezwa kupitia makubaliano maalum yaliyosainiwa kati ya Benki ya Ushirika na Kampuni ya CMC Agri, taasisi inayojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa zana za kilimo, kwa lengo la kuwapatia wakulima, vyama vya ushirika na wadau wa mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula fursa ya kupata teknolojia na zana za kisasa kwa mfumo wa malipo ya awamu.

Kwa mujibu wa Ng’urah, ushirikiano huo utarahisisha upatikanaji wa vifaa vitakavyowawezesha wakulima kuongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali za kilimo ikiwemo umwagiliaji, upaliliaji, uvunaji, uchakataji, ufungashaji na uhifadhi wa mazao.

Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia hizo yatasaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo pamoja na kuimarisha uwezo wa wakulima kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Tunataka kuona wakulima wanapata zana na teknolojia zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji na kuhamia katika kilimo cha kibiashara chenye tija,” amesema Ng’urah.

Aidha, amesema Benki ya Ushirika inalenga kufikia zaidi ya wateja wadogo 10,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo mikopo na huduma za akaunti, hatua itakayosaidia kuwaunganisha wakulima wengi zaidi na fursa za kifedha.

Amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za kukuza sekta ya kilimo na kuwawezesha wakulima nchini kutumia fursa zinazotokana na teknolojia na huduma jumuishi za kifedha.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...