Na Mwandishi Wetu

Meneja Kanda ya Kati wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Bi. Hawa Lweno, ametoa wito kwa mafundi umeme kutembelea banda la Mamlaka hiyo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela jijini Dodoma, ili kupata elimu kuhusu umuhimu wa kupata leseni za ufundi umeme zinazotolewa na EWURA, pamoja na utaratibu wa kuomba leseni hizo.

Amesema kuwa leseni za ufundi umeme ni muhimu katika kuhakikisha huduma za ufungaji, ukarabati na matengenezo ya mifumo ya umeme zinafanywa na mafundi wenye sifa na wanaozingatia viwango vya ubora na usalama, hivyo kupunguza ajali zinazoweza kusababishwa na kazi za umeme zisizokidhi matakwa ya kitaalamu.

“Hili linaendana sambamba na wito kwa wananchi kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mifumo yao ya umeme kila baada ya miaka mitano tangu mfumo huo ulipofungwa,” ameeleza.

Bi. Lweno amesema EWURA pia inatumia Maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuongeza matumizi ya nishati safi kwa Watanzania.

Aidha, maeneo mengine yanayotolewa elimu ni pamoja na fursa za uwekezaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini, taratibu za kuwasilisha na kushughulikia malalamiko yanayohusu huduma zinazodhibitiwa na EWURA, pamoja na matumizi salama ya huduma za mafuta, umeme na gesi.

     

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...