Na Janeth Raphael - MichuziTv

PWANI: Tanzania imeingia katika hatua mpya ya sekta ya nishati baada ya Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) kuzinduliwa rasmi, huku mradi huo ukitarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo leo, Jumamosi, Agosti 22, 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa JNHPP ni matokeo ya msimamo wa Serikali wa kuwekeza katika miradi mikubwa yenye uwezo wa kubadilisha mazingira ya uzalishaji na upatikanaji wa umeme nchini.

Rais Samia amesema mradi huo una umuhimu wa kipekee kwa Tanzania kutokana na uwezo wake wa kuongeza uzalishaji wa umeme, akisisitiza kuwa Serikali haikuwa na sababu ya kuacha kuutekeleza kwa kuzingatia mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Rais Samia, amesema hatua ya sasa imefikiwa baada ya safari ndefu ya utekelezaji wa mradi huo, akirejea Desemba 22, 2022 aliposhuhudia hatua ya kufungwa kwa njia ya kuchepusha maji ya Mto Rufiji na kuanza kwa ujazaji wa bwawa.

Amesema awali ilitarajiwa bwawa hilo kujazwa ndani ya kipindi cha takribani miaka mitatu, lakini kutokana na kasi ya ujazaji maji, lilifikia kiwango kilichowezesha majaribio ya uzalishaji wa umeme ndani ya takribani mwaka mmoja na nusu.

Katika ziara yake wakati wa uzinduzi, Rais Samia alikagua miundombinu mbalimbali ya mradi huo, ikiwemo mitambo ya kuzalisha umeme, tuta kuu pamoja na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kwenda kwenye Gridi ya Taifa.

Amesema kuona miundombinu hiyo ikifanya kazi ni hatua kubwa na ya kujivunia kwa Tanzania, hasa kutokana na nafasi ya mradi huo katika kuimarisha uwezo wa nchi kukidhi mahitaji ya umeme yanayoongezeka.

JNHPP ina uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, kiwango kinachoongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini.

Ongezeko hilo linatarajiwa kutoa msukumo kwa sekta mbalimbali, ikiwemo viwanda, biashara, uwekezaji na huduma za kijamii, huku upatikanaji wa umeme wa uhakika ukiendelea kuwa msingi muhimu wa ukuaji wa uchumi.

Kwa kukamilika na kuzinduliwa kwa JNHPP, Tanzania sasa inaongeza uwezo wake wa kuzalisha umeme na kuweka mazingira bora zaidi ya kukabiliana na mahitaji ya nishati yanayoendelea kukua.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...