Na Pamela Mollel,Mererani Simanjiro
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika teknolojia za kisasa za utafiti wa madini ili kuongeza uzalishaji, kubaini maeneo mapya yenye rasilimali na kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na utajiri wake wa madini
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, anasema teknolojia ya kisasa ndiyo msingi muhimu wa kuleta mapinduzi katika sekta ya madini, hasa katika utafiti na uchimbaji wa rasilimali zilizopo chini ya ardhi kwa ufanisi na tija kubwa
Mhe. Mavunde ameyasema hayo Agosti 24, 2026, wakati wa ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya Tanzanite katika eneo la Mererani, Wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, ambako alitembelea kampuni ya Franone Mining & Gems Co. Ltd na Chusa Mining Limited
Anasema Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa za utafiti ili kupata taarifa sahihi kuhusu miamba na maeneo yenye madini, hatua itakayosaidia wachimbaji kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuwekeza katika shughuli za uchimbaji
Waziri huyo anasema kwa kutumia teknolojia, utafiti wa madini unaweza kufanyika kwa ufanisi zaidi na kutoa majibu ya kisayansi kuhusu maeneo yenye rasilimali, hivyo kuongeza nafasi ya kugundua na kufungua maeneo mapya ya uzalishaji wa madini nchini
Ameongeza kuwa katika historia ya Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan ameandika historia kwa kuweka mazingira yatakayowezesha fedha zinazotokana na sekta ya madini kuelekezwa katika kazi za utafiti, kwa lengo la kuongeza maeneo mapya ya uzalishaji wa madini mbalimbali nchini, ikiwemo Tanzanite
Aidha Mh Mavunde,anasema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mkubwa wa Serikali wa kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kuendeleza sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Taifa
Anasema kipaumbele cha kwanza katika mkakati huo ni eneo la Mererani, kutokana na kuwa na madini ya Tanzanite, madini adimu ambayo hayapatikani popote duniani
Ameongeza kuwa Serikali ina wajibu mkubwa wa kuyatunza, kuyahifadhi na kuhakikisha rasilimali hiyo inawanufaisha Watanzania na vizazi vijavyo
“Kipaumbele cha kwanza ni eneo la Mererani, ambapo kuna madini adimu ambayo hayapatikani popote duniani Lazima tuyalinde na kuyatunza, huku tukihakikisha yanaendelea kuchangia maendeleo ya Taifa letu,” anasema Mhe. Mavunde.
Waziri Mavunde ameipongeza kampuni ya Franone Mining & Gems Co. Ltd kwa kutumia teknolojia katika kuimarisha usimamizi na shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na Chusa Mining Limited kwa kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo
Anasema hatua za kampuni hizo zinapaswa kuwa mfano kwa wawekezaji wengine, huku Serikali ikiendelea kuwahimiza kutumia teknolojia za kisasa kuongeza ufanisi, usalama na uzalishaji wa madini nchini.



.jpeg)

.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...