Na Mashaka Mhando, Muheza

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC), Mohammed Salim 'Ratco', amewataka wasimamizi wa miradi ya maendeleo wilayani Muheza kuhakikisha kunakuwepo na thamani halisi ya fedha (Value for Money) kwenye miradi, ili kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo badala ya maneno.

Ratco ametoa agizo hilo Leo Augosti 1, wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Tanga iliyofanya ukaguzi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Misozwe, wilayani humo.

Alisisitiza kuwa, kutokana na Rais Dkt. Samia kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya wananchi, kuna kila sababu ya kuhakikisha miradi hiyo inajengwa kwa viwango stahiki na fedha zinatumika kwa makusudio yaliyotarajiwa.

"Tuwe tunamshukuru Rais wetu kwa vitendo, tusimshukuru kwa maneno. Fedha zinazotolewa na Serikali zifanye kazi iliyotarajiwa na kuleta tija kwa wananchi wetu," alisisitiza MNEC huyo.

Katika majumuisho ya ziara hiyo yaliyofanyika eneo la Kwabastola, Ratco alibainisha kuwa ingawa ujenzi wa kituo hicho unaendelea vizuri na umefikia asilimia 68, wasimamizi wanapaswa kuwa makini na kurekebisha mapungufu madogo madogo yaliyoonekana mapema.

Akikazia maelekezo hayo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tanga, Swaibu Mwanyoka, aliwasihi wasimamizi kuepuka kufanya kazi kimazoea na badala yake wawe waadilifu katika usimamizi wao ili kuepuka hasara.

Awali, akiwasilisha taarifa ya ujenzi huo unaotarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 14, 2026, Mganga Mkuu wa Zahanati ya Misozwe, Rukia Kashegu, alisema mradi huo unagharimu kiasi cha Shilingi Milioni 250.

Rukia alifafanua kuwa mradi huo uliopo Kijiji cha Manyoni, Tarafa ya Ngomeni, unajumuisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD), choo cha nje cha wagonjwa, pamoja na miundombinu ya taka za hospitali.

Aliongeza kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zilizomo ndani ya Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030, yenye lengo la kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora itakayowawezesha kushiriki vyema katika shughuli za ujenzi wa taifa.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...