Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Imani kwamba haki inaweza kufuatiliwa na kupatikana bila kujali hali ya mtu imeongezeka kwa familia moja kutoka Meru mkoani Arusha, baada ya kupata msaada kupitia Programu ya “Sema na Waziri” ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Familia hiyo ilikuwa imekumbwa na changamoto baada ya kuacha kazi ya ualimu katika shule ya msingi ambako walikuwa wakijitolea kufundisha, huku ikiwa bado inadai stahiki zake. Changamoto hiyo iliwasilishwa kupitia programu hiyo na kuanza kufanyiwa kazi na watumishi wa Wizara.

Ufuatiliaji uliofanywa na Wizara kwa kuwasiliana na wahusika umefanikisha familia hiyo kupata stahiki zilizokuwa zikidaiwa, hatua ambayo imeelezwa kuwa imewapa matumaini mapya kuhusu upatikanaji wa haki.

Akizungumza katika programu hiyo, Lidya Ernest kutoka Meru, Arusha, amesema awali alikuwa na mtazamo kwamba haki ilikuwa rahisi kupatikana zaidi kwa watu wenye uwezo, lakini uzoefu walioupata umebadili mtazamo huo.

“Nitumie nafasi hii kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka Programu ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa ajili ya kutusaidia Watanzania wote bila kuangalia matabaka wala nyadhifa, wala hali ya mtu. Hata sisi watu wa huku chini nasi tumefikiwa,” amesema Lidya.

Kwa mujibu wa Lidya, hatua hiyo imewapa yeye na mume wake ujasiri wa kuendelea kufuatilia haki zao kupitia njia sahihi, huku wakitambua umuhimu wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Katiba na Sheria imewakabidhi Lidya na mume wake Sh milioni 1.5, fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuwawezesha kuanzisha shughuli za ujasiriamali na kujikwamua kiuchumi.

Msaada huo unalenga kuwapa fursa ya kutumia fedha hizo kama mtaji wa shughuli za uzalishaji, hatua inayotarajiwa kusaidia familia hiyo kujenga chanzo cha kipato na kuimarisha maisha yao.

Tukio hilo limeonyesha pia nafasi ya Programu ya “Sema na Waziri” katika kuwapa wananchi jukwaa la kuwasilisha changamoto zao za kisheria na kupata ufuatiliaji kutoka kwa Wizara.

Kwa familia hiyo kutoka Meru, msaada walioupata haujaishia katika kurejeshewa stahiki walizokuwa wakidai, bali umeenda sambamba na kupata mtaji wa kuanza shughuli za ujasiriamali, jambo ambalo wameeleza kuwa limewapa matumaini mapya ya kujikwamua kiuchumi.

Hatua hiyo pia inaendelea kuimarisha ujumbe kwamba upatikanaji wa haki haupaswi kuwa fursa ya wachache, bali huduma inayopaswa kuwafikia wananchi wote bila kujali uwezo wao, hadhi au nafasi zao katika jamii.


Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...