Na Janeth Raphael - MichuziTv

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amezitaka Kamati za Ushauri wa Stadi (TACs) za Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira, teknolojia na mabadiliko ya sekta mbalimbali. Prof. Mkenda amesema mafunzo ya ufundi stadi hayapaswi kuishia katika utoaji wa vyeti, bali yanapaswa kumwandaa mhitimu kuwa na ujuzi, umahiri, ubunifu, nidhamu ya kazi na uwezo wa kutumia teknolojia katika kufanya kazi na kujiajiri.

Akizungumza leo Agosti 13, 2026, jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Kamati hizo, Prof. Mkenda amesema TACs zinapaswa kuwa “macho na masikio” ya VETA kwa kufuatilia mabadiliko ya teknolojia, uzalishaji na mahitaji ya waajiri katika maeneo ya kazi. Amesisitiza kuwa kamati hizo zisibaki kuwa za mikutano pekee, bali ziwe za matokeo kwa kutoa ushauri wa wakati kuhusu maboresho ya mitaala, kuanzishwa kwa stadi mpya na kuondolewa kwa teknolojia zilizopitwa na wakati.

Waziri Mkenda amesema ushauri wa TACs ni muhimu katika kuhakikisha vijana wanaohitimu wanakuwa na ujuzi unaohitajika na waajiri, huku VETA ikipata fursa ya kuanzisha programu mpya katika sekta zenye fursa za ajira na kujiajiri, ikiwemo TEHAMA, utalii, ukarimu, sanaa, ujenzi, nishati, kilimo na uzalishaji. Amesema waajiri wanapaswa kuwa sehemu ya mfumo wa mafunzo kwa kueleza mahitaji yao ya ujuzi, vifaa, teknolojia na viwango vya utendaji vinavyohitajika.

Akihusisha hatua hiyo na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Prof. Mkenda amesema Tanzania haiwezi kuwa na uchumi imara, jumuishi na shindani bila kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi. Amesema elimu na mafunzo ya ufundi stadi ni nyenzo muhimu katika kujenga viwanda vya kisasa, uchumi wa kidijitali na uwezo wa Taifa kuzalisha bidhaa na huduma kwa kutumia maarifa, teknolojia na ubunifu wa ndani.

Aidha, Prof. Mkenda amesema kuanzishwa kwa TACs ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, inayosisitiza elimu inayokidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa na soko la ajira. Ameeleza pia kuwa Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu na sekta ya viwanda kupitia Mpango wa Kitaifa wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Sekta ya Viwanda katika Ukuzaji wa Ujuzi na Uwezeshaji wa Ajira, uliozinduliwa Februari 9, 2026, jijini Dar es Salaam.

Prof. Mkenda amewataka wajumbe wa TACs kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi, ubunifu, uwajibikaji na uzalendo, huku wakiwa mabalozi wa VETA katika sekta zao na kuhamasisha waajiri kushirikiana na taasisi hiyo katika kuandaa mitaala, kutoa mafunzo kwa vitendo, kuboresha teknolojia na kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi unaohitajika. Amesisitiza kuwa utekelezaji wa Dira 2050 hautategemea mipango na nyaraka pekee, bali Watanzania wenye maarifa, ujuzi, ubunifu, nidhamu na uwezo wa kutumia teknolojia.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...