Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Husna Sekiboko, ametoa wito wa kuimarishwa kwa elimu na mafunzo ya ufundi na ujasiriamali nchini, akisema ujuzi wa vitendo unaweza kuwa silaha muhimu kwa vijana katika kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa kujiajiri na kuunda ajira kwa wengine.

Amesema hayo akiwa kwenye banda la VETA katika Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Jijini Tanga.

Sekiboko amesema badala ya vijana kuhitimu na kuendelea kusubiri ajira, wanapaswa kutumia ujuzi wanaoupata katika vyuo vya ufundi kuanzisha shughuli za uzalishaji, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha kupata vitendea kazi, mitaji na masoko.

Amesema changamoto ya ukosefu wa ajira inahitaji suluhisho linalowafanya vijana kuwa sehemu ya uzalishaji, akisisitiza kuwa kijana mwenye ujuzi ana uwezo wa kujiajiri na baadaye kuwa mwajiri wa wengine.

“Ni bora kijana kuanza na kile kidogo alichonacho na kujenga shughuli yake mwenyewe, kwa sababu anaweza kujiajiri na baadaye kuajiri wengine. Kwa kufanya hivyo, anakuwa amefanya zaidi kwa ajili yake mwenyewe na jamii yake kuliko kusubiri ajira pekee,” amesema.

Ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea banda la VETA na kukutana na vijana na wanachuo na wahitimu wa VETA ambapo amesema ameona uwezo mkubwa walionao katika kutengeneza bidhaa na kutoa huduma zinazoweza kukidhi mahitaji ya jamii.

Kwa mujibu wa Sekiboko, vyuo vya ufundi stadi vina nafasi kubwa katika utekelezaji wa jitihada za kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa sababu vinawapatia vijana ujuzi wa vitendo ambao unaweza kutumika moja kwa moja katika uzalishaji.

Amesema ili ujuzi huo uwe na matokeo makubwa zaidi, vijana wanahitaji mazingira mazuri ya kujifunzia, vifaa vya kufanyia kazi na fursa za kupata mitaji ili kugeuza ujuzi wao kuwa biashara na ajira.

Amehimiza vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali na taasisi mbalimbali kupata ujuzi na mitaji, akisema mtaji mdogo unaweza kuwa mwanzo wa shughuli kubwa endapo utatumika vizuri.

“Lengo ni kuondokana na utamaduni wa kusubiri ajira pekee. Kijana akipata ujuzi, anaweza kuutumia kuzalisha ajira yeye mwenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa katika taasisi,” amesema.

Amesema hatua hiyo pia inaweza kusaidia kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kwa kuongeza idadi ya vijana wanaoshiriki katika uzalishaji na kujenga uchumi kupitia ujuzi, ubunifu na ujasiriamali.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...