
Na TAEC Dodoma
Kila mwaka tarehe 29 Agosti, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Majaribio ya Nyuklia (International Day against Nuclear Tests), ikiwa ni fursa ya kutafakari madhara yaliyosababishwa na majaribio ya silaha za nyuklia na kuendelea kuhimiza juhudi za kujenga dunia yenye amani na usalama.
Siku hii ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2009 kupitia Azimio Na. 64/35, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu madhara ya majaribio ya silaha za nyuklia na umuhimu wa kuyasitisha. Tarehe 29 Agosti pia ina umuhimu wa kihistoria kutokana na kufungwa kwa eneo la majaribio ya nyuklia la Semipalatinsk nchini Kazakhstan mwaka 1991.
Tangu jaribio la kwanza la silaha ya nyuklia mwaka 1945, zaidi ya majaribio 2,000 yamefanyika duniani, yakiacha historia ya madhara kwa afya ya binadamu, mazingira na usalama wa dunia.
Katika kuadhimisha siku hii, Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) inaungana na jumuiya ya kimataifa kupinga majaribio ya silaha za nyuklia na kusisitiza matumizi salama, yenye uwajibikaji na ya amani ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.
Ni muhimu kuelewa kuwa kupinga majaribio ya silaha za nyuklia si kupinga teknolojia ya nyuklia. Teknolojia hii inapotumika kwa madhumuni ya amani na chini ya mifumo madhubuti ya usalama na udhibiti, ina mchango mkubwa katika kuboresha maisha na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Nchini Tanzania, TAEC ina jukumu la kusimamia na kudhibiti matumizi salama ya vyanzo vya mionzi pamoja na kuhamasisha matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, kilimo, mifugo, viwanda, migodi, maji, utafiti, mazingira na nishati.
Katika afya, teknolojia ya mionzi inatumika katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali; katika kilimo na mifugo inachangia katika utafiti, uboreshaji wa uzalishaji na udhibiti wa baadhi ya wadudu na magonjwa. Mbinu za nyuklia pia zina matumizi muhimu katika tafiti za rasilimali za maji, viwanda, migodi na maeneo mengine ya maendeleo.
Kwa msingi huo, tunapaswa kutofautisha kati ya matumizi ya nyuklia kwa madhumuni ya kijeshi na matumizi yake kwa madhumuni ya amani. Hofu inayotokana na madhara ya silaha za nyuklia isiwe sababu ya kuiona teknolojia yote ya nyuklia kama tishio.
TAEC itaendelea kuhakikisha matumizi ya vyanzo vya mionzi nchini yanafanyika kwa kuzingatia sheria na viwango vya usalama ili kuwalinda wafanyakazi, wagonjwa, wananchi na mazingira. Tutaendelea pia kutoa elimu kwa umma ili kuondoa dhana potofu na kuongeza uelewa kuhusu manufaa ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.
Tunapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Majaribio ya Nyuklia, tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kupata taarifa sahihi na kuunga mkono matumizi salama na ya amani ya teknolojia ya nyuklia kwa manufaa ya Taifa na ustawi wa binadamu.
Ujumbe wetu ni wazi: HAPANA kwa majaribio ya silaha za nyuklia; NDIYO kwa matumizi salama na ya amani ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo ya Taifa.
“Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa.”


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...