Na Belinda Joseph-Dodoma.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma limefanya kikao kikao kazi na Maafisa wa Jeshi la Polisi ngazi ya kata, wilaya na Mkoa wa Dodoma, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa miundombinu ya umeme na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Kurwa Mangara, amesema ushirikishwaji wa vyombo vya ulinzi ni muhimu kutokana na nafasi ya umeme katika maisha ya wananchi na shughuli za kiuchumi.
Amesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na changamoto za uhujumu na uharibifu wa miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, ikiwemo wizi wa vyuma na bolti pamoja na uvamizi wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya njia za kusafirisha umeme.
Mangara ameeleza kuwa baadhi ya maeneo hayo yamekuwa yakitumika kwa shughuli za kilimo na uchimbaji wa mchanga na kokoto, hali inayoweza kusababisha mmomonyoko wa udongo na kuhatarisha nguzo pamoja na miundombinu mingine ya umeme.
Aidha, ametaja changamoto ya kuibiwa nyaya zinazotumika kulinda transfoma na kuchomwa kwa nguzo za umeme wakati wa uandaaji wa mashamba vitendo ambavyo vinaweza kusababisha kukatika kwa umeme, hasara kwa TANESCO na usumbufu kwa wananchi.
Ametoa wito kwa wananchi kutambua thamani ya miundombinu ya umeme na kuacha vitendo vinavyoweza kuhatarisha upatikanaji wa nishati hiyo, akisisitiza kuwa ulinzi wa miundombinu ya umeme ni jukumu la pamoja kwa TANESCO, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa wa Jeshi la Polisi ASP Regina Mtana, amewashukuru TANESCO kwa kutoa elimu hiyo na kuahidi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na shirika hilo katika kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya umeme na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na upatikanaji wa nishati hiyo.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...