Na Belinda Joseph-Tanga

Serikali imeanza mchakato wa kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha uhakiki wa malori ya mafuta katika Mkoa wa Tanga, hatua inayolenga kuwaondolea wafanyabiashara usumbufu, muda na gharama za kusafiri hadi Mkoa wa Pwani kupata huduma hiyo.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Tanga, Julius Temba, leo Agosti 18, 2026, wakati akizungumza katika mwendelezo wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea jijini Tanga.

Temba amesema mchakato huo umeanza katika mwaka wa fedha 2026/2027 baada ya Serikali kutambua changamoto inayowakabili wafanyabiashara wa malori ya mafuta wanaohitaji huduma ya uhakiki.

Amesema kwa sasa, wafanyabiashara kutoka Tanga hulazimika kusafiri hadi eneo la Misugusugu, Mkoa wa Pwani, kwa ajili ya kuhakiki malori yao, hali inayoongeza gharama na muda wa kupata huduma hiyo.

Amesema kituo hicho kinatarajiwa kujengwa katika eneo litakalokuwa kwenye barabara ya Segera kuelekea Tanga, na kikikamilika kitasaidia kurahisisha huduma ya uhakiki wa malori ya mafuta kwa wafanyabiashara wa Tanga na maeneo jirani.

Amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya watu kutumia vipimo visivyo sahihi, hivyo Wakala unaendelea kutoa elimu na kuimarisha ufuatiliaji ili kuhakikisha wananchi wanatumia vipimo vinavyokidhi viwango vinavyotakiwa.

Amesema kupitia maonesho hayo, WMA inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi, huku ikiendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za vipimo mkoani Tanga.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...