Na Janeth Raphael -MichuziTv
Tanzania imeendelea kuimarisha hadhi yake katika sekta ya mbegu barani Afrika baada ya kushika nafasi ya tatu kati ya nchi 55 kwa ubora wa mifumo ya mbegu, huku juhudi za kudhibiti mbegu feki na zisizokidhi viwango zikiongezwa ili kulinda maslahi ya wakulima na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Mafanikio hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Nyasebwa Chimangu, ambaye amesema hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika usimamizi wa ubora wa mbegu zimeifanya Tanzania kuendelea kuwa mfano katika bara la Afrika.
Kwa mujibu wa Chimangu, mafanikio hayo yametokana na kuimarishwa kwa ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya mbegu, maghala ya kuhifadhi pamoja na viwanda vya kuchakata mbegu, kwa kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na vyombo vya ulinzi na usalama.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, jumla ya watu na taasisi 22 zilizobainika kukiuka Sheria ya Mbegu zilichukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani, kutozwa faini na kuwalipa fidia wakulima waliopata hasara kutokana na matumizi ya mbegu zisizokidhi viwango.
"Tanzania imepata alama 7.25 kati ya 10 katika tathmini ya The African Seed Access Index (TASAI) ya mwaka 2023 na kushika nafasi ya tatu barani Afrika, nyuma ya Afrika Kusini iliyopata alama 8.62 na Zambia yenye alama 7.89," amesema Chimangu.
Amefafanua kuwa nafasi hiyo imechangiwa na kuimarika kwa sheria na sera za mbegu, ubora wa vifungashio, mfumo wa usajili wa aina mpya za mbegu, maendeleo ya mifumo ya mbegu inayosimamiwa na wakulima pamoja na kukua kwa biashara ya mbegu ndani na nje ya Tanzania.
Mbali na mafanikio hayo, Tanzania imeendelea kudumisha ithibati ya kimataifa ya International Seed Testing Association (ISTA), na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi 14 za Afrika na 80 duniani zenye maabara zilizoidhinishwa kufanya upimaji wa ubora wa mbegu kwa viwango vya kimataifa.
Chimangu amesema ithibati hiyo imeipa TOSCI uwezo wa kutoa vyeti vya ISTA Orange International Certificate (OIC) kwa mbegu zinazouzwa katika masoko ya kimataifa, hatua ambayo imeongeza imani ya wawekezaji na kuvutia kampuni za kimataifa za uzalishaji na biashara ya mbegu, ambazo sasa zimefikia takribani 29 nchini.
Aidha, amesema Tanzania inaendelea kuwa mwanachama wa Skimu za Mbegu za Shirika la OECD, ikiwa ni miongoni mwa nchi 10 pekee za Afrika zinazoshiriki katika mfumo huo wa kimataifa, jambo linaloongeza ushindani wa mbegu zinazozalishwa nchini na kufungua masoko mapya ya kimataifa.
Katika mwaka wa fedha 2025/2026 pekee, TOSCI ilitoa vibali 392 vya kusafirisha nje ya nchi tani 993.21 za mbegu. Kati ya kiasi hicho, tani 722.20 zilikuwa mbegu za mikunde, tani 204.07 za nafaka, tani 55.44 za mazao ya bustani na tani 11.50 za mazao ya mafuta, takwimu zinazoonyesha kuendelea kukua kwa uzalishaji na biashara ya mbegu za Tanzania katika soko la dunia.
Hatua hizo zinaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora barani Afrika, huku zikichochea ongezeko la tija kwa wakulima na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa Taifa.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...