Na Belinda Joseph-Tanga
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imebuni programu ya simu ya Afya Kijani inayolenga kuwasaidia wakulima kutambua magonjwa ya mazao kwa kutumia picha kupitia teknolojia ya akili unde yakiwa bado shambani.
Akizungumza Salvatory Mwesige Eustace, mtafiti na mbunifu kutoka TARI Ukiriguru, Mwanza, amesema programu hiyo itamwezesha mkulima kupiga picha ya mmea wenye dalili za ugonjwa kwa kutumia simu yake, kisha kupata taarifa kuhusu aina ya ugonjwa unaoathiri zao hilo.
Amesema baada ya kutambua ugonjwa, programu hiyo pia itatoa mapendekezo ya hatua ambazo mkulima anapaswa kuchukua ili kuzuia au kutibu ugonjwa huo, huku ikitarajiwa kuunganishwa na maafisa ugani kwa ajili ya kutoa ushauri zaidi kwa wakulima.
“Afya Kiliani itamsaidia mkulima kutambua ugonjwa uliopo shambani na kumpa mapendekezo ya namna ya kuuzuia au kutibu, hivyo kupunguza upotevu wa mazao unaotokana na kutokujua aina ya ugonjwa unaoharibu mazao."
Amesema kwa sasa programu hiyo iko katika hatua ya majaribio shambani, huku ikitarajiwa kuanza kupatikana kwa umma kupitia Play Store na App Store baada ya kukamilika kwa majaribio yanayoendelea.
Mwesige amesema katika hatua ya awali, watafiti wamekusanya sampuli za pamba zenye magonjwa tofauti, ikiwemo bacteria na sampuli hizo zimeingizwa kwenye mfumo ili kuuwezesha kutambua magonjwa hayo kupitia picha.
Amesema ubunifu huo umechukua takribani miezi sita kufanyiwa kazi, huku TARI ikiendelea kuuboresha ili kuongeza uwezo wa programu hiyo, ikiwemo kutoa taarifa za hali ya hewa ya eneo husika na kusaidia mkulima kupanga shughuli zake za kilimo.
Akieleza sababu ya kushiriki katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Kitaifa inayofanyika Tanga, Mwesige amesema TARI imetumia jukwaa hilo kuwaonyesha wananchi, hususan wakulima, namna teknolojia na ubunifu vinavyoweza kutumika kutatua changamoto zinazowakabili katika kilimo.
Amesema ni muhimu wakulima kutumia mbinu bora za kilimo badala ya kutegemea nguvu kazi pekee, akiwataka kutumia fursa zinazotolewa na watafiti na wabunifu ili kuongeza uzalishaji na kipato.
“Kilimo cha sasa hakiwezi kutegemea nguvu nyingi pekee yake, Wakulima wanahitaji mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji".
Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Kitaifa inafanyika Tanga kunzia tarehe 15 hadi 24, ikiwa ni jukwaa la kuwaunganisha watafiti, vyuo, wabunifu, wanafunzi na wadau wa elimu, katika kuonesha teknolojia na suluhisho mbalimbali zinazolenga kuchochea maendeleo ya jamii.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...