Na Mashaka Mhando, Handeni
HATUA ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwezesha makundi maalum kiuchumi imeanza kuzaa matunda makubwa Wilayani Handeni, baada ya kikundi cha vijana waliokuwa madereva, makondakta, na wapiga debe eneo la Mkata kufanikiwa kununua gari la abiria aina ya Toyota Coaster.
Mafanikio hayo makubwa yamefikiwa kupitia mkopo wa Shilingi Milioni 90 utokanao na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Taarifa ya mafanikio ya vijana hao imetolewa Leo Augosti 1, mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Tanga, wakiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Bw. Mohammed Salim, waliokuwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo unaomilikiwa na kikundi hicho cha vijana cha Mkata, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Saitoti Stephen, alisema mradi mzima unagharimu Shilingi Milioni 100.
Saitoti alifafanua kuwa, kati ya fedha hizo, Shilingi Milioni 10 zilitokana na mtaji wa vijana wenyewe waliokuwa wakijishughulisha na uwakala wa usafirishaji, huku Shilingi Milioni 90 zikiwa ni mkopo usio na riba kutoka halmashauri.
"Kabla ya kuwakabidhi fedha hizi, Halmashauri iliwapeleka vijana hawa kwenye ziara ya kimkakati ya kimafunzo eneo la Chalinze ili kuwajengea uwezo wa kibiashara. Tunafurahi kuona mradi huu sasa unazalisha ajira na kuwawezesha vijana hawa kulea familia zao," alieleza Saitoti.
Rekodi ya Marejesho
Katika hatua inayothibitisha uaminifu na dhamira ya vijana hao, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa tayari wameanza kufanya marejesho kulingana na mkataba wao, ambapo mpaka sasa kiasi cha Shilingi Milioni 6.3 kimekwisha rejeshwa serikalini.
Alisema mafanikio hayo na uaminifu ulioonyeshwa umechangiwa kwa kiasi kikubwa na Jukwaa la Vijana la Wilaya ya Handeni, ambalo limekuwa likihamasisha uadilifu, uzalendo, na kutunza amani, sambamba na kuwahamasisha vijana wengine kuchangamkia fursa za kiuchumi.
Mkurugenzi Saitoti alihitimisha kwa kutoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa makusudi wa kuendelea kutoa mabilioni ya fedha yanayoleta mageuzi ya kiuchumi na kupunguza wimbi la vijana wanaozurura mitaani.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...