Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ametoa maelekezo manne kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), akilitaka kuhakikisha Awamu ya Pili ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako (Fiber to the Home – FTTH) inawanufaisha wananchi kwa kuwapatia huduma yenye ubora, uhakika na gharama nafuu.

Waziri Kairuki ametoa maelekezo hayo Agosti 21,2026, wakati akizindua rasmi utekelezaji wa Awamu ya Pili ya mradi huo katika Ukumbi wa Johari Rotana, Dar es Salaam, akisisitiza kuwa mafanikio ya mradi hayapaswi kupimwa kwa idadi ya Home Pass au miundombinu iliyojengwa pekee, bali kwa idadi ya wateja wanaounganishwa, ubora wa huduma, kasi ya intaneti na kuridhika kwa wateja.

Ametaka TTCL kupanua wigo wa huduma ya faiba kwa kuhakikisha inafika katika maeneo yenye makazi yanayokua, masoko, maeneo ya biashara, viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.

Pili, ameitaka TTCL kudumisha ubora wa huduma na kuimarisha huduma kwa wateja, ikiwemo kuhakikisha malalamiko yanashughulikiwa kwa haraka na kwa ufanisi.

Tatu, Waziri Kairuki amelitaka Shirika kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa gharama nafuu kwa kuandaa vifurushi vinavyokidhi uwezo wa familia, wanafunzi, vijana na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Nne, amesisitiza uwajibikaji na nidhamu ya kibiashara katika usimamizi wa mradi, akitaka wazabuni na wakandarasi wasimamiwe kwa ufanisi ili kazi zikamilike kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha inayowekezwa.

Waziri Kairuki amesema Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako si ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano pekee, bali ni hatua ya kimkakati ya kufungua fursa za elimu, biashara, ajira na ubunifu, sambamba na kuchochea ujenzi wa uchumi wa kidijitali nchini.

Amesema mradi huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali 2024–2034, unaolenga kuongeza matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa huduma za Serikali kwa njia ya kidijitali.

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, Lengo Namba Nne la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 linakusudia kuhakikisha ifikapo mwaka 2050 angalau asilimia 70 ya wananchi wanatumia TEHAMA, huku zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali zikipatikana kwa njia ya kidijitali iliyo salama na jumuishi.

Akitumia takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa robo mwaka iliyoishia Juni 2026, Waziri Kairuki amesema usajili wa intaneti nchini umefikia 62,793,986, huku matumizi ya data yakifikia Petabaiti 1,041.

Hata hivyo, amesema usajili wa huduma ya Faiba Nyumbani ulikuwa 178,904, hali inayoonyesha kuwa bado kuna fursa kubwa ya kukuza huduma ya intaneti ya kasi kupitia teknolojia ya nyuzi za macho.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA Moremi Marwa, amesema Awamu ya Pili ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Biashara wa Miaka 10 wa Shirika kwa kipindi cha 2025/26 hadi 2034/35, unaolenga kuimarisha na kuboresha huduma za mawasiliano nchini.

Marwa amesema TTCL imeingia katika Awamu ya Pili ikiwa tayari imejenga msingi muhimu kupitia utekelezaji wa Awamu ya Kwanza, iliyolenga maeneo mbalimbali ya kimkakati nchini.

Amesema katika Awamu ya Kwanza, TTCL imefanikiwa kujenga zaidi ya Home Pass 280,000, huku jumla ya maungio ya huduma ya nyuzi za macho yakifikia karibu 300,000 nchini.

Kwa upande wa Awamu ya Pili, amesema TTCL inalenga kuongeza zaidi ya Home Pass 400,000, hatua inayotarajiwa kupanua wigo wa upatikanaji wa intaneti ya kasi kwa wananchi, taasisi na wafanyabiashara.

Marwa amesema TTCL katika utekelezaji wa Awamu ya Pili imeendelea kutumia teknolojia ya kisasa ya Gigabit Passive Optical Network (GPON) badala ya mfumo wa Point-to-Point uliokuwa ukitumika awali.

Amesema teknolojia hiyo inawezesha TTCL kuwahudumia wateja wengi kwa wakati mmoja, kuongeza ufanisi wa matumizi ya miundombinu, kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha ubora wa huduma za intaneti.

Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yanaipa TTCL uwezo wa kutumia miundombinu ya nyuzi za macho kwa ufanisi zaidi na kuongeza uwezo wa kutoa huduma ya intaneti yenye kasi na uhakika kwa watumiaji.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa ushirikiano na makandarasi wa ndani na wa kimataifa, wakiwemo Huawei, ZTT na Visoll, katika ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya nyuzi za macho.

Amesema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha upanuzi wa mtandao unafanyika kwa kutumia teknolojia za kisasa na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za intaneti nchini.

Marwa amesema Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako ililenga maeneo mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Geita, Iringa, Mbeya na Mwanza, pamoja na Unguja, Zanzibar.

Amesema mafanikio yaliyopatikana katika awamu hiyo yameiwezesha TTCL kuendelea na upanuzi wa miundombinu kupitia Awamu ya Pili, huku ikilenga kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Mradi huo unalenga pia kuchochea matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku, biashara, elimu na huduma za Serikali, sambamba na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia upatikanaji wa intaneti yenye kasi na uhakika.

Waziri Kairuki amewataka wananchi kutumia fursa hiyo katika kujifunza, kufanya biashara, kuongeza uzalishaji, kubuni fursa mpya za ajira na kupata huduma za Serikali kwa njia ya kidijitali.

Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda miundombinu ya mawasiliano dhidi ya uharibifu na wizi, ili kuhakikisha uwekezaji huo unaendelea kutoa huduma bora na kuchangia maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...