Shirika la Aga Khan Foundation limeeleza umuhimu wa miradi ya maendeleo katika kujenga uwezo wa jamii na kuwawezesha wanufaika kujitegemea ili shughuli zao ziweze kuendelea hata baada ya ufadhili wa wafadhili kumalizika.

Akichangia mjadala Septemba 24, kuhusu kutoka utegemezi wa wafadhili kuelekea uendelevu wa rasilimali za ndani katika Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Dodoma na Tuzo za Ubunifu 2026, Afisa Mradi wa Tuinuke Pamoja unaotekelezwa na Aga Khan Foundation, Nahumu Fungo, amesema miradi inapaswa kujikita katika kuwajengea uwezo watu wa ngazi ya chini ili waweze kuendelea na shughuli za maendeleo kwa kutumia fursa na rasilimali zinazopatikana katika jamii zao.

Fungo amesema kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja unaolenga kukuza usawa wa kijinsia, Aga Khan Foundation imekuwa ikitumia uwezeshaji wa kiuchumi kama sehemu ya kuwawezesha wanawake kuongeza vipato, akieleza kuwa shirika hilo hushirikiana na mashirika mbalimbali kulingana na mahitaji ya jamii na vikundi husika, ikiwemo kuwaunganisha na bidhaa za kampuni ili kujenga ushirikiano unaoweza kuendelea hata baada ya mradi kukamilika.

Katika jukwaa hilo lililofanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Fikra Mpya kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kupitia Vyanzo vya Ndani,” Aga Khan Foundation imetunukiwa Tuzo ya Women Empowerment kwa kutambua mchango wake kupitia utekelezaji wa Mradi wa Tuinuke Pamoja katika kuwawezesha wanawake wa Mkoa wa Dodoma kiuchumi na kutoa elimu kuhusu usawa wa kijinsia, chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Khatibu Kazungu, amezitaka mashirika yasiyo ya kiserikali kuzingatia masharti ya sheria, kushiriki mikutano na vikao vya wadau, kuwasilisha kwa wakati taarifa za robo mwaka na mwaka pamoja na kulipa ada kwa wakati.

Kazungu pia amesisitiza mashirika hayo kulinda maslahi ya nchi, kuheshimu mila, desturi, utamaduni na maadili, kuhakikisha wanufaika wanashirikishwa katika utekelezaji wa miradi na kuzingatia mipango na vipaumbele vya Serikali, hususan Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Kwa upande wake, Patrick Mafuru, akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, amesisitiza mashirika kufanya kazi kwa ushirikiano na kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazowaongoza, akieleza kuwa lengo kuu linapaswa kuwa kuisaidia Serikali kufikisha huduma kwa jamii katika maeneo ambayo bado haijafika.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...