Mkurugenzi wa Shirika la INADES Formation Tanzania, Jacqueline Nicodemus, amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuweka mikakati ya kuwa na vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuhakikisha yanaendelea kutekeleza shughuli zake bila kutegemea zaidi fedha kutoka kwa wafadhili.

Akizungumza leo Septemba 24, 2026, jijini Dodoma kwenye Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Dodoma, amesema ushiriki wao katika jukwaa hilo ulianza katika ngazi za wilaya, ambapo walishiriki katika majukwaa yaliyofanyika katika wilaya tano kabla ya kufikia ngazi ya mkoa.

Amesema ajenda kubwa iliyojadiliwa ni uendelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, hususan changamoto ya kuwa na vyanzo vya kutosha vya mapato ili kupunguza utegemezi wa fedha kutoka kwa wafadhili.

Aidha, amesema mashirika yanaweza kutumia fursa zilizopo kuendeleza bidhaa na huduma mbalimbali zinazoweza kuzalisha mapato, hatua ambayo itasaidia kupanua wigo wa mapato na kuimarisha utekelezaji wa shughuli zao.

Kwa upande mwingine, amesema kupitia majukwaa hayo, wadau wameweza kujadili na kuweka mikakati ya kuhakikisha mashirika yanapata fursa zaidi za mapato na kuwa na uwezo wa kujiendesha kwa uendelevu.

Ameongeza kuwa mjadala huo utaendelea katika ngazi ya kitaifa mwezi Oktoba, ambapo mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka maeneo mbalimbali Nchini yataendelea kutoa mchango kuhusu namna ya kujenga uendelevu wa sekta hiyo nchini Tanzania.

Naye Rajab A. Rajab, ambaye ni mjumbe wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali NACONGO, kutoka Wilaya ya Kondoa, ameeleza kuwa INADES Formation Tanzania imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo mazingira, kilimo, ufugaji, elimu na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Amesema kupitia shughuli za mazingira, shirika hilo limefanikiwa kupanda zaidi ya miti 80,000 katika mkoa wa Dodoma, huku likiendelea kuwafikia wakulima na wafugaji kwa kutoa elimu na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Aidha, amesema katika maeneo ambayo shirika halifiki moja kwa moja, hutumia njia mbalimbali kuwafikishia wananchi elimu na taarifa muhimu, ikiwemo tafiti na machapisho yanayowasaidia wakulima kupata uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.

Ameeleza pia kuwa matokeo ya shughuli za shirika yanaonesha kuwa zaidi ya vikundi saba vinaendelea kutekeleza shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini, huku vikifikia zaidi ya watu 150,000.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Khatibu Kazungu, amezitaka mashirika yasiyo ya kiserikali kuzingatia masharti ya sheria, kushiriki mikutano na vikao vya wadau, kuwasilisha kwa wakati taarifa za robo mwaka na mwaka pamoja na kulipa ada kwa wakati.

Kazungu pia amesisitiza mashirika hayo kulinda maslahi ya nchi, kuheshimu mila, desturi, utamaduni na maadili, kuhakikisha wanufaika wanashirikishwa katika utekelezaji wa miradi na kuzingatia mipango na vipaumbele vya Serikali, hususan Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Kwa upande wake, Patrick Mafuru, akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, amesisitiza mashirika kufanya kazi kwa ushirikiano na kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazowaongoza, akieleza kuwa lengo kuu linapaswa kuwa kuisaidia Serikali kufikisha huduma kwa jamii katika maeneo ambayo bado haijafika.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...