Na Janeth Raphael -MichuziTv

Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imetangaza matokeo ya Mitihani ya Kati Awamu ya Pili ya Taaluma ya Ununuzi na Ugavi iliyofanyika nchini kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 4, 2026, huku watahiniwa 275 kati ya 528 waliofanya mitihani hiyo wakifaulu.

Akizungumza leo, Septemba 18, 2026, jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, amesema mitihani hiyo imeendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na. 23 ya mwaka 2007 iliyoanzisha Bodi hiyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kuendesha mafunzo na mitihani ya kitaaluma katika fani ya Ununuzi na Ugavi.

Amesema jumla ya watahiniwa 567 walidahiliwa kufanya mitihani hiyo, ambapo watahiniwa 528 sawa na asilimia 93.1 walifanya mitihani, huku 39 wakikosa kwa sababu mbalimbali.

Mbanyi amesema kati ya watahiniwa 528 waliofanya mitihani, 275 sawa na asilimia 52.1 wamefaulu, watahiniwa 232 sawa na asilimia 43.9 wamepewa nafasi ya kurudia masomo yao, huku 21 sawa na asilimia 4.1 wakifeli na kutakiwa kuanza upya masomo katika ngazi husika.

Mbanyi ametoa pongezi kwa watahiniwa waliofaulu katika ngazi mbalimbali, wakiwemo waliokidhi vigezo vya kutunukiwa vyeti vya Professional Diploma, Graduate Professional na CPSP, huku akiwapongeza pia wahadhiri na wakufunzi kutoka vyuo na vituo vya mafunzo kwa mchango wao katika kuwaandaa watahiniwa.

Aidha, amesema PSPTB inawaalika watahiniwa waliokamilisha sifa za Professional Diploma I na II, Graduate Professional I, II na III pamoja na Research kushiriki katika Mahafali ya 15 ya Bodi yatakayofanyika kwa ajili ya kutunuku sifa hizo.

Katika hatua nyingine, Mbanyi amewataka watahiniwa ambao hawakufaulu kujisajili na kurudia masomo yao katika Mitihani ya Kati itakayofanyika kuanzia Novemba 9 hadi 13, 2026. Amesema dirisha la usajili limefunguliwa tangu Septemba 8 na litafungwa Oktoba 24, 2026, huku watahiniwa wenye referral status ya nafasi ya mwisho wakitakiwa kutumia mitihani ya Novemba vizuri, kwani baada ya muda huo hadhi hiyo itaondolewa kwa mujibu wa mtaala wa Bodi.

PSPTB pia imewahimiza wanafunzi waliomaliza vyuo vikuu ndani na nje ya Tanzania kujisajili kwa ajili ya mitihani ya kitaaluma ya Bodi ili kupata sifa stahiki katika fani ya Ununuzi na Ugavi. Wazazi, wadhamini na waajiri nao wametakiwa kuwaunga mkono watahiniwa kwa kugharamia ada za maandalizi na mitihani, hatua ambayo itasaidia kuongeza idadi ya wataalamu wenye maarifa na ujuzi katika sekta hiyo muhimu.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...