Na Janeth Raphael - MichuziTv

Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kwa kuongeza uwezo wa kitaaluma na kuboresha miundombinu yake, hatua inayolenga kuifanya taasisi hiyo kuwa na uwezo mkubwa zaidi katika kutoa elimu, kufanya tafiti, ubunifu na uzalishaji wa maarifa.

Katika kuimarisha rasilimali watu, Serikali imeiwezesha TIA kupata Maprofesa tisa pamoja na kufadhili watumishi 78 kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) ndani na nje ya nchi. Kati ya watumishi hao, 48 tayari wamehitimu masomo yao, huku 30 wakiendelea na masomo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Amos Pallangyo, amesema hatua hiyo imeongeza idadi ya wataalamu wenye sifa za juu za kitaaluma na kuimarisha uwezo wa taasisi hiyo katika ufundishaji, utafiti, ubunifu na uzalishaji wa maarifa.

Amesema ongezeko hilo la uwezo wa kitaaluma limekwenda sambamba na upanuzi wa fursa za elimu ya juu, ambapo TIA imeweza kuanzisha programu za Shahada ya Uzamili katika kampasi zake za Zanzibar, Mbeya, Singida na Mwanza, hatua inayowezesha wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini kupata fursa zaidi za elimu ya juu.

Prof. Pallangyo amesema mafanikio hayo yamechochewa pia na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu ya elimu, ambapo katika kipindi cha miaka mitano jumla ya Shilingi bilioni 67.9 zimewekezwa katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu katika kampasi za TIA zilizopo Mtwara, Mbeya, Singida, Kigoma, Mwanza na Zanzibar.

Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 27.8 zimetolewa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Fedha hizo zimetumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu, TEHAMA, samani, mafunzo ya wahadhiri, maboresho ya mitaala, tathmini na shughuli nyingine za mradi.

Katika fedha hizo za HEET, Shilingi bilioni 22.6 zimeelekezwa moja kwa moja katika ujenzi wa miundombinu ya kampasi za Singida na Mwanza. Kwa upande wa Singida, ujenzi wa jengo la taaluma umefikia asilimia 72 na unatarajiwa kukamilika Septemba 28, 2026. Mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 14.7 unatarajiwa kuongeza uwezo wa kampasi hiyo kuhudumia wanafunzi hadi 3,650 na tayari umezalisha ajira 275.

Amesema katika Kampasi ya Mwanza, ujenzi wa mabweni kupitia mradi wa HEET umefikia asilimia 96. Mabweni hayo yatakapokamilika yataweza kuhudumia wanafunzi 306, wakiwemo wanawake 203 na wanaume 103, huku mradi huo ukiwa umegharimu Shilingi bilioni 7.9 na kuzalisha ajira 323.

Mbali na uwekezaji kupitia HEET, Serikali kupitia Wizara ya Fedha imewekeza Shilingi bilioni 45.2 katika miradi mbalimbali ya TIA katika kampasi za Mwanza, Kigoma, Zanzibar, Mbeya na Mtwara.

Katika Kampasi ya Mwanza, jengo la taaluma na utawala limekamilika na linaendelea kutumika, likiwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,620 kwa wakati mmoja. Ujenzi wa jengo hilo umegharimu Shilingi bilioni 8.4 na umezalisha ajira 223.

Kampasi ya Kigoma nayo imepiga hatua ambapo jengo la taaluma na utawala limefikia asilimia 98 na tayari linatumika. Mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 11.5 umezalisha ajira 217.

Kwa upande wa Zanzibar, ujenzi wa jengo la taaluma, utawala na mabweni umefikia asilimia 45 na unaendelea. Mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 16.3 umezalisha ajira 130 hadi sasa na utakapokamilika utawezesha TIA kudahili wanafunzi 580 na kutoa huduma ya mabweni kwa wanafunzi 480.

Katika Kampasi ya Mbeya, ujenzi wa jengo lenye kumbi za mihadhara, maktaba na maabara ya kompyuta umekamilika kwa asilimia 100 na tayari linatumika. Jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 250 katika kumbi za mihadhara, wanafunzi 180 katika maktaba na wanafunzi 168 katika maabara ya kompyuta. Mradi huo umegharimu Shilingi bilioni 3.4 na umezalisha ajira 110.

Kwa upande wa Mtwara, Serikali imekamilisha ujenzi wa jengo la taaluma, maktaba, maabara ya kompyuta, mabweni pamoja na nyumba za watumishi. Mradi huo umegharimu Shilingi bilioni 5.6 na umezalisha ajira 334 wakati wa utekelezaji wake.

Miundombinu hiyo ina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 175 katika maabara ya kompyuta, 200 katika maktaba na wanafunzi 650 katika madarasa manne. Aidha, mabweni yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 324, wakiwemo wanaume 212 na wanawake 112.

Prof. Pallangyo amesema uwekezaji huo mkubwa wa Serikali haujalenga kuboresha majengo ya TIA pekee, bali umeongeza uwezo wa taasisi hiyo kuhudumia wanafunzi wengi zaidi, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuimarisha shughuli za kitaaluma na uzalishaji wa maarifa.

Amesema pia uwekezaji huo umeleta manufaa kwa jamii zinazozunguka kampasi hizo kwa kuchochea shughuli za kiuchumi, ikiwemo kuibua fursa za ajira na biashara ndogo ndogo kwa wananchi.

Prof. Pallangyo ameyasema hayo jijini Dodoma, Septemba 7, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO kuhusu utekelezaji wa TIA katika mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na mwelekeo wa taasisi hiyo katika mwaka wa fedha 2026/27.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...