Na Mwandishi Wetu
USHIRIKIANO kati ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Taasisi ya Zanzibar ya Uhasibu, Ukaguzi na Ushauri wa Kodi (ZIAAT) unatarajiwa kuongeza fursa za mafunzo, kuimarisha weledi wa wataalamu na kuchangia usimamizi bora wa fedha na huduma kwa umma.
Taasisi hizo zimetia saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) leo, Septemba 1, 2026, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kitaalamu. Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William A. Pallangyo, amesema ushirikiano huo utawezesha taasisi hizo kutumia kwa pamoja utaalamu na rasilimali katika kuendeleza wataalamu.
Maeneo ya ushirikiano ni pamoja na mafunzo ya Certified Tax Technician (CTT), Maendeleo Endelevu ya Kitaaluma (CPD), usimamizi wa vituo vya mitihani vya CTT na CTP, tafiti, machapisho na mikutano ya kitaaluma, pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu wa sekta ya fedha na utumishi wa umma.
Kwa wananchi na wataalamu, ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza fursa za mafunzo na maendeleo ya kitaaluma, kukuza wataalamu wenye ujuzi na weledi zaidi, pamoja na kuibua tafiti na maarifa yatakayosaidia kutatua changamoto za jamii.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa ZIAAT, CPA Ame Burhan Shadhil, ameipongeza TIA kwa kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kuahidi kuendelea kushirikiana katika kuendeleza wahasibu, wakaguzi na watafiti. Amesema ushirikiano huo utasaidia kuimarisha weledi na uadilifu wa wataalamu na watumishi wa umma.
Kwa ujumla, makubaliano hayo yanaweka msingi wa kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, weledi na uadilifu zaidi, kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kuchangia utoaji wa huduma bora kwa wananchi, sambamba na juhudi za kufikia Dira ya Taifa 2050.



.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...