Dar es Salaam
Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limeungana na Serikali kutoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuchukua tahadhari na kufanya maandalizi ya mapema dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
TRAMEPRO limesema uzoefu wa matukio yaliyopita unaonesha kuwa mvua kubwa zinapokutana na makazi yaliyo katika maeneo hatarishi, mifumo dhaifu ya mifereji, uharibifu wa mazingira na maandalizi duni, madhara yanaweza kuwa makubwa.
Kwa mujibu wa shirika hilo, mafuriko yanaweza kusababisha vifo na uharibifu wa nyumba pamoja na miundombinu ikiwemo barabara, madaraja, shule na hospitali, huku yakiathiri pia kilimo, biashara, upatikanaji wa maji na nishati.
TRAMEPRO pia imeonya kuwa uchafuzi wa maji unaoweza kutokea wakati wa mafuriko unaweza kuongeza hatari ya magonjwa na changamoto za afya ya jamii.
Shirika hilo limeeleza kuwa El Niño ni mfumo wa asili unaoweza kubadilisha mwenendo wa hali ya hewa, na athari zake hutofautiana kati ya tukio moja na jingine.
Katika maandalizi hayo, TRAMEPRO imetoa wito kwa mamlaka za mikoa, wilaya na halmashauri kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, mifereji ya maji, miundombinu na mipango ya uokoaji pamoja na kutambua maeneo hatarishi.
Aidha, limevitaka vyama vya siasa kuweka tofauti zao pembeni katika masuala ya usalama wa wananchi na kutumia nafasi zao kuelimisha jamii kuhusu tahadhari, utunzaji wa mazingira na maandalizi dhidi ya majanga.
TRAMEPRO pia imewataka viongozi wa dini na viongozi wa mila na desturi kutumia nafasi zao kuhamasisha jamii kuhusu usafi wa mazingira, matumizi salama ya maji, utunzaji wa misitu, vyanzo vya maji, mito na maeneo oevu.
Katika sekta ya elimu, shirika hilo limezitaka shule, vyuo na taasisi za elimu kuwa na mipango ya usalama kwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wakati wa mvua kubwa, pamoja na kuwafundisha namna ya kuchukua tahadhari wakati wa mafuriko na radi.
Kwa upande wa afya, TRAMEPRO imesisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema kwa ajili ya ongezeko la mahitaji ya huduma za afya, kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha usafi wa chakula na maji.
Wananchi nao wametakiwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika, kuepuka kuvuka mito au maeneo yenye maji mengi na kutokujenga katika maeneo hatarishi.
TRAMEPRO imesisitiza kuwa maandalizi ya mapema yanaweza kusaidia kuokoa maisha na kupunguza madhara wakati wa majanga.
“El Niño si sababu ya hofu; ni sababu ya maandalizi. Tahadhari ya mapema ni kinga ya maisha. Taarifa sahihi ni sehemu ya uokoaji. Umoja wetu ndiyo nguvu yetu,” limeeleza shirika hilo.
TRAMEPRO imeongeza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuhamasisha jamii kuhusu afya, mazingira, usalama wa jamii na matumizi sahihi ya maarifa ya asili katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo imetolewa na Boniventura Mwalongo, Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, jijini Dar es Salaam.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...